NIDA Yasaidia Kupunguza Riba za Benki
Na: Thomas Nyakabengwe, NIDA
MIAKA ya hivi karibuni riba imeendelea kushuka kwenye benki za biashara hapa nchini. Kushuka kwa riba si miujiza bali kumetokana na jitihada mbalimbali za Serikali hususan katika udhibiti wa sekta ya fedha. Moja ya jitihada hizo za Serikali ni kuhakikisha suala la utambuzi wa watu linafanyika kwa kuanzisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambayo inafanya kazi adhimu ya Usajili na Utambuzi wa Watu. Kuwapo kwa NIDA ambayo pamoja na majukumu ya usajili na utambuzi wa watu, imetekeleza pia jukumu la kujenga Kanzidata ya Taarifa za Watu ambazo zinatumika kitaifa na kimataifa. Kanzidata ya NIDA inaweza kushirikishana taarifa na mifumo ya taasisi nyingine zikiwamo benki na hivyo kuwezesha taasisi hizo kutambua wateja wake kielektroniki (eKYC). Kuwezeshwa kwa benki kutambua wateja wake kielektroniki kumepunguza hofu au wasiwasi wa kutambua wateja wake hasa wanaoomba mikopo.
Kabla ya kuwapo Mfumo wa Usajili na Utambuzi wa Watu, taasisi za fedha hasa benki zilikuwa zinapata changamoto ya kuwatambua wateja wake na hivyo kutokuwa na uhakika na taarifa wanazotoa wakati wanapoomba mikopo.
Lakini hivi sasa benki zinaweza kuwatambua wateja kirahisi kwa kutumia mfumo wa NIDA ambao una taarifa zote muhimu za wateja ambazo benki zinahitaji ili kumtambua mteja. Kupungua kwa changomoto ya utambuzi wa wateja kumeziwezesha benki kupunguza riba hadi kufikia asilia 15 (15%) kwa mikopo tofauti na zaidi ya asilimia 17 (17%) kwa mwaka kwa miaka ya nyuma. Kuimarika kwa utambuzi wa wateja pia kumeziwezesha benki kuongeza riba kwa wateja wa akaunti za akiba “Saving Account” kwani hivi sasa wanapata asilimia tatu (3%) na zaidi tofauti na asiliamia moja (1%) kwa mwaka kwa miaka ya nyuma.
Hivyo, kuwapo kwa Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu unaosimamiwa na NIDA kumeleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya fedha kwa kupunguza vihatarishi vya kuwaamini wateja wa benki wanaomba mikopo na kuwaamini wateja wanaoweka fedha benki.
Wananchi wengi kuwa na sifa za kukopesheka na kuaminiwa na taasisi za fedha ni hatua kubwa ya kuinua uchumi wa nchi kwa sababu wanapata mitaji ya kuwekeza kwenye shughuli mbalimbali za uchumi. Kuongezeka kwa riba kwenye akaunti za akiba ni kivutio kwa wananchi kuweka fedha zao benki badala kuweka kwenye vibubu majumbani. Riba kwenye benki za Tanzania zinaweza kushuka zaidi kama mfumuko wa bei duniani utaendelea kushuka kwa sababu kwenye eneo la kutambua wateja hakuna changamoto tena.