Historia ya NIDA
-
1968
Wazo la kuanzisha Vitambulisho vya Taifa
Wazo la kuanzisha Vitambulisho vya Taifa kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoishi nchini Tanzania lilizaliwa mwaka 1968 katika kikao cha 'Interstate Intelligence Gathering' kilichojumuisha wajumbe kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia. Kwa wakati huo nchi za Kenya na Zambia tayari zilikuwa na Vitambulisho vyao vya Taifa. Iliazimiwa kwamba ili kuimarisha mahusiano ya kiusalama yanayozingatia Utawala wa Sheria katika nchi hizo nne ni lazima nchi za Uganda na Tanzania nazo zikatoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia wao.
Kumekuwa na jitihada mbalimbali za Serikali kuhakikisha Watanzania na wageni wote wanapatiwa Vitambulisho vya Taifa, lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda yaliyotajariwa kwa kipindi kirefu kutokana na sababu mbalimbali. Mwaka 1986 Serikali ilitunga Sheria ya Vitambulisho ambayo haikutumika wala kutungiwa kanuni zake.
-
2006
Upembuzi yakinifu wa Vitambulisho vya Taifa
Upembuzi yakinifu wa Vitambulisho vya Taifa uliofanyika mwaka 2006 ulidhihirisha kuwa mradi wa vitambulisho vya Taifa unatekelezeka. Aidha taarifa hiyo iliainisha makadirio ya gharama za mradi na namna mradi utakavyotekelezwa ambapo teknolojia ya 'Smartcard' ndiyo itakayotumika kama ilivyokubaliwa na Baraza la Mawaziri katika kikao kilichokaa mjini Dodoma mwezi Februari, 2007.
Aidha katika Kikao chake cha tarehe 03 Februari, 2007 Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo kuwa iundwe Kamati ya Usimamizi (Steering Committee) ya Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara na Vitengo vinavyohusika na mambo muhimu kuhusu Vitambulisho vya Taifa. Kamati hiyo pamoja na mambo mengine itakuwa na jukumu la kutoa mwongozo na mwelekeo wa programu za Mradi.
Baada ya azimio la kikao hicho, mwaka 1986 Serikali ilitunga Sheria ya Vitambulisho vya Taifa ambayo haikutumika. Mwaka 2012 ilifanyiwa mapitio na kutungiwa kanuni zake mwaka 2014.
-
2008
kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia Vitambulisho vya Taifa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wa serikali ya awamu ya nne, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alitia saini Hati ya kuidhinisha kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia Vitambulisho vya Taifa kinachojulikana kama Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (National Identification Authority (NIDA). Hati hiyo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali, GN No.122 ya tarehe 01 Agosti, 2008 ambapo NIDA ilikasimishwa majukumu kadhaa yakiwemo ya:
Kutambua na Kusajili wakazi wote wanaoishi nchini wenye umri wa miaka 18 na zaidi na kuandikisha taarifa zao ambazo zinatambulika kitaifa na kimataifa
kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia, wageni wakaazi na wakimbizi wote wanaoishi nchini kihalali vinavyoweza kutumika kitaifa na kimataifa
kusimamia na kuendeleza Utawala Bora wa Mamlaka sambamba na
kusimamia uanzishaji na utunzaji wa Daftari Kuu la Taifa la Kielektroniki lenye kuhifadhi taarifa sahihi za watu wote wanaoishi nchini, za kuaminika na rahisi kuzipata pindi zinapohitajika kutumika na mifumo mingine ya serikali na sekta binafsi.
Ni wazi kwamba kwa wakati huu kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na Vitambulisho vya Taifa kulingana na mazingira yaliyopo. Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo nchi tano zimeungana na kukubaliana kwamba watu wa nchi hizo wanaweza kutembeleana bila bughudha pia kumeongeza umuhimu wa kuwa na Vitambulisho vya Taifa. Sababu hiyo imepelekea NIDA kujizatiti na kuhakikisha imefungua ofisi za Usajili katika wilaya zote nchini bara na visiwani Zanzibar ili kutoa huduma za Usajili na Utambuzi wa Watu kwa wananchi wa pande zote.
-
2011
Kuanza kwa Shughuli ya Usajili na Utambuzi wa Watu
Shughuli ya Usajili na Utambuzi wa Watu ilianza mwaka 2011 kwa watumishi wa umma na kwa wananchi wa wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya majaribio na baadae kuanza Usajili rasmi katika mkoa wa Dar Es Salaam Juni, 2012 na baadae kusambaza huduma ya Usajili na Utambuzi wa Watu katika wilaya zote za Tanzania bara na visiwani Zanzibar ambapo hadi sasa NIDA ina ofisi za Usajili wilayani zipatazo 151.