Yajue Makundi na Mahitaji ya Kurekebisha Taarifa Zisizo Sahihi NIDA
Na Mwandishi Wetu-NIDA
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kwa miaka kadhaa nyuma ilipokea maombi ya mabadiliko ya taarifa ambayo yalishindikana kufanyiwa marekebisho husika, kutokana na kukinzana na Sheria, Taratibu, Kanuni na Miongozo ya Usajili na Utambuzi wa Watu iliyopo.
Kutokana na changamoto hiyo NIDA iliomba kibali maalum cha kuruhusu mabadiliko ya taarifa hizo kufanyika. Ilipotimu Oktoba 2025, Serikali ilitoa kibali hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kufanyia kazi maombi yote ya mabadiliko ya taarifa kwa watu ambao waliwasilisha taarifa za kughushi na za udanganyifu.
“Lengo hasa la msamaha huo kutolewa ni kuhakikisha Taifa linakuwa na kanzi data iliyobeba taarifa sahihi, madhubuti na za kuaminika za watu wote wanaoishi Tanzania kihalali, ili ziweze kutumika katika taasisi za Serikali na binafsi wakati wa kutoa huduma kwa wananchi pasipo kuhatarisha usalama wa raia, mali zao na taifa kwa ujumla”. alisema James Kaji, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) alipokuwa akiutaarifu umma kupitia vyombo vya habari siku za hivi karibuni.
Kibali hicho kimehusisha makundi manne (4). Kundi la kwanza ni waathirika wa vyeti vya kughushi, waliofukuzwa katika ajira za Serikali kutokana na kutumia vyeti vya shule vya kughushi.
Ili kufanyiwa marekebisho kwenye taarifa zao, watu wa kundi hili wanatakiwa kuwasilisha viambatisho vya lazima vifuatavyo; barua ya ajira katika Utumishi wa Umma; barua ya kufukuzwa kazi katika Utumishi wa Umma; nakala ya vyeti halisi vya elimu; cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Hati ya kubadili jina (Deed poll) iliyosajiliwa na Gazeti la Serikali.
Kundi la pili ni la watu waliotumia taarifa za watu wengine kupata vyeti vya elimu pamoja na watu walioajiriwa na kustaafu kwa majina ya watu wengine. Viambatisho vya lazima ambavyo wanatakiwa kuwasilisha NIDA ni pamoja na cheti cha kidato cha nne; uthibitisho wa umiliki halali wa cheti cha kidato cha nne kutoka NECTA; vyeti vya elimu; cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na RITA, barua ya kustaafu, kitambulisho cha mfuko wa jamii na deed poll iliyosajiliwa na gazeti la Serikali.
Kibali pia kimeainisha kundi la tatu ni lile linalowahusu watu waliotoa taarifa za udanganyifu na kuambatisha nyaraka zisizo sahihi katika usajili wa NIDA kutokana na sababu mbalimbali walizozijua wao. Wahusika watatakiwa kukiri katika barua za maombi kuwa walifanya udanganyifu na kwamba wanaomba taarifa sahihi ndiyo zitumike katika kanzidata ya NIDA.
Mahitaji ya kundi hili ni pamoja na kuwasilisha vyeti vya elimu, cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na RITA na deed poll iliyosajiliwa na gazeti la Serikali.
Kundi la mwisho ni la raia wa Tanzania waliojisajili kwa hadhi ya ukimbizi. Kundi hili linahusisha waliosajiliwa NIDA kwa kuweka nyaraka za ukimbizi wakati ni raia wa Tanzania.
Watu hao watatakiwa kuwasilisha viambatisho vya lazima ambavyo ni barua ya uthibitisho wa uraia kutoka Idara ya Uhamiaji; vyeti vya elimu, cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na RITA, hati ya kubadili jina (Deed poll) iliyosajiliwa na gazeti la Serikali.
Aidha, kwa makundi yote manne, watatakiwa kuwasilisha viambatisho vya ziada walivyonavyo kati ya leseni ya udereva, kadi ya mpiga kura, Hati ya kusafiria, kadi ya bima ya afya, leseni ya udereva, cheti cha Namba ya Mlipa Kodi (TIN), kadi ya mpiga kura au cheti cha ndoa.
“NIDA ina uwezo wa kumtaka muhusika awasilishe nyaraka au kielelezo chochote cha ziada kitakachohitajika mbali na vilivyoainishwa hapo juu”. Amesema Kaji.
Mkurugenzi Mkuu amehitimisha mazungumzo yake kwa kuhimiza wananchi waliodanganya taarifa zao kujitokeza mapema kutumia fursa hii ya msamaha wa Mhe. Rais wa mwaka mmoja ambayo ameitoa ili kurekebisha taarifa zao kabla ya mud…

