emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe


Wageni Ruksa Kumiliki Vitambulisho vya Taifa

Na Thomas Nyakabengwe-NIDA 

Wageni wanaoishi kihalali Tanzania wanatakiwa kuwa na Vitambulisho vya Taifa kulingana na hadhi zao.

Wanaostahili kuwa na vitambulisho ni Wageni Wakaazi wenye umri wa miaka 18 na zaidi, wanaoishi nchini kwa zaidi ya miezi sita ambao wana vibali vya ukaazi na kufanya kazi.

Kundi jingine ni la Wakimbizi wanaotambuliwa na Idara ya Huduma kwa Wakimbizi iliyopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

Kumiliki vitambulisho kwa wageni ni takwa la kisheria ambalo linaelekeza wageni wote wanaoishi nchini kutambuliwa kulingana na hadhi zao. 

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji alisema Mamlaka hiyo inatoa vitambulisho vya aina tatu ambavyo ni vya raia, wageni wakaazi na wakimbizi. 

Alisema kuna tofauti kati ya vitambulisho vya raia na wageni kwa sababu kila kimoja kimeandikwa hadhi yake (raia, mgeni mkaazi au mkimbizi) na vya raia havina ukomo wa matumizi wakati vya wageni huhuishwa au huisha kulingana na ukomo wa vibali vya ukaazi au kazi (residence and work permit).