NIDA Ndio Maisha
Na Thomas W. Nyakabengwe-NIDA
“NIDA ndio kila kitu, NIDA ndio maisha. Kitambulisho cha Taifa ndio Utaifa wenyewe.” Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, James Kaji alipozungumza na Waandishi wa Habari Novemba 27, 2025, Makao Makuu ya NIDA, Dar es Salaam.
Kauli hizi za Kaji zinalenga kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa katika maisha ya kila siku ya Mtanzania.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba ili upate huduma mbalimbali hapa nchini na hata nje, ni lazima utambulike kama ni Mtanzania kweli na namna ya pekee ya kumtambua mtu ni lazima awe amesajiliwa na kutambuliwa na NIDA na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) au na Kitambulisho cha Taifa.
NIDA imekuwa taasisi wezeshi kupata huduma mbalimbali kama vile kujiunga na ngazi mbalimbali za elimu, mikopo, kusajili laini za simu, kufungua akaunti benki, kufungua kampuni, kumiliki ardhi, kusafiri, kupata dhamana, kupata bima ya afya, pamoja na kupata pensheni na mafao. Hivyo, kuwa na NIDA ni kama kuwa na Ufunguo wa Maisha ya Kitaifa na Kimataifa.
Neno maisha lina maana nyingi na mawanda mapana lakini maana yake kwa muktadha wa kawaida ni masuala makuu kuhusu thamani, madhumuni na umuhimu wa binadamu kuwepo duniani. Hivyo, kuwa na Kitambulisho cha Taifa ambacho ni wezeshi kupata huduma mbalimbali ni kuwa na maisha.
Kinyume cha maana hiyo ni kukosa lengo, kuwepo bure, kutokuwa na maana kunakomfanya mtu ajisikie mnyonge, pengine kukata tamaa ya kuishi.

