emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe


Vitambulisho vya Raia Havina Mwisho wa Matumizi

Na Mwandishi Wetu-NIDA

Wananchi wameendelea kunufaika na uamuzi wa Serikali wa kuondoa ukomo wa matumizi ya Vitambulisho vya Taifa na sasa vitambulisho hivyo vinaendelea kutumika kwenye taasisi za Serikali na sekta binafsi wanapokwenda kupata huduma za kijamii na kiuchumi. 

Akijibu maswali kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, alifafanua kwamba hilo lilifanyiwa kazi na viongozi wenzake waliotangulia NIDA na utekelezaji wake unaendelea.

“Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (MOHA), imeshaondoa ukomo wa matumizi ya Kitambulisho cha Taifa hivyo wananchi waendelee kutumia vitambulisho vyao pindi wanapohitaji huduma za kijamii na kiuchumi katika taasisi za Serikali na binafsi.” alisema.

Manufaa hayo yametokana na Serikali ya Awamu ya Sita kuwa sikivu kwa kupokea maoni yaliyotolewa na wananchi na kuamua Kanuni za Sheria Na. 11 ya Usajili na Utambuzi wa Watu kufanyiwa marekebisho Februari 21, 2023 na kutoa kibali kwa Raia wa Tanzania kuendelea kutumia Vitambulisho vya Taifa bila ukomo. 

Sambamba na hilo, taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi zilielekezwa kuendelea kuvitambua vitambulisho hivyo wakati wa kuwahudumia wananchi. 

Ikumbukwe tarehe ya ukomo wa matumizi ya vitambulisho hauwahusu wageni wakaazi na wakimbizi, wao wanaendelea na utaratibu wa kuhuisha taarifa zao kulingana na utaratibu uliowekwa na NIDA.