emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe


Vitambulisho vya Taifa Havitolewi Kiholela

Na Mwandishi wetu - NIDA 


Vitambulisho vya Taifa havitolewi papohapo kama vitambulisho vingine kwa sababu mchakato wa utolewaji wake unahitaji uchujaji wa kina wa taarifa za waombaji unaohusisha taasisi mbalimbali za Serikali. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, James Kaji katika mahojiano na waandishi wa habari, yaliyofanyika Dar es Salaam hivi karibuni. 


“Vitambulisho vya Taifa ni suala la kiusalama zaidi. Hivyo, havitolewi kiholela kwa hasa kwa maombi yenye kutiliwa shaka, maombi yote lazima yafanyiwe uhakiki wa taarifa za kuzaliwa, makazi, uraia na kibaiolojia za mwombaji na uhakiki ni suala endelevu” Alisema Mkurugenzi Mkuu.


Wananchi wanaojisajili na kukidhi vigezo vya Maombi ya Utambulisho wa Taifa, hupatiwa Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) ndani ya siku tano na Kitambulisho cha Taifa ndani ya siku 21. 


Aliendelea kufafanua kuwa, ili kuimarisha udhibiti vitambulisho visitolewe kiholela, vitambulisho vyote vinachapishwa kwenye kituo kimoja. Lakini mwananchi anaposajiliwa ana uhuru wa kuchagua wilaya ya kupokelea kitambulisho chake na asipotumia fursa hiyo kujieleza wakati anasajiliwa, kitambulisho chake kikishachapishwa kitapelekwa katika wilaya aliyojisajilia.


Amesema suala la usalama na uraia linapewa kipaumbele zaidi, ndio maana uhakiki ni endelevu hata kwa waliopatiwa NIN na vitambulisho. Ikigundulika kuwa Namba ya Utambulisho au Kitambulisho cha Taifa kimetolewa kwa mtu ambaye hana sifa au vigezo vya kupatiwa kitambulisho husika, kulingana na aina ya vitambulisho vinavyofahamika kisheria, Namba hiyo au kitambulisho hicho kitafungiwa au kuzuiwa matumizi hadi pale mhusika atakapokuja NIDA ili kuhakiki taarifa za umiliki wa Kitambulisho husika kama ilivyofanyika katika baadhi ya maeneo hasa yaliyopo mipakani mwa nchi.