Wanahabari Watakiwa Kuelimisha Umma Kuhusu Utambulisho
Na Alphani Mlacha-NIDA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamkala ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji amewataka wanahabari kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujisajili na kutambua umuhimu wa uraia wao kwa kujisajili kwenye mfumo wa utambuzi uliopo chini ya NIDA.
Rai hiyo imetolewa na Kaji, Novemba 27, 2025 alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya NIDA, jijini Dar es Salaam.
“Ndugu zangu wanahabari naomba mtumie vyombo vyenu kuelimisha wananchi juu ya kujisajili kwenye Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu na kuhusu taarifa muhimu zitolewazo na NIDA’’alisema Kaji.
Alisema kuwa kwa muda huu NIDA ni maisha hutaweza kufanya shughuli yoyote bila ya kuwa na namba ya NIDA au Kitambulisho cha Taifa ni muhimu kila mwananchi kujisajili ili aweze kupatiwa namba na baadaye kitambulisho ili kimsaidie katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi ikiwemo kufungua akaunti za kibenki kupata hati za kusafiria, leseni za udereva pamoja na biashara.
Sambamba na hilo alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa sahihi wakati wa kujisajili ili kuwa na taarifa sahihi kwenye kanzi data na kuonya kwamba kutoa taarifa zisizo sahihi ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu.
Alisisitiza kuwa kwa sasa mwombaji wa kitambulisho anapata Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) ndani ya siku tano na baada ya siku 21 anapata Kitambulisho cha Taifa.

