4R za Rais Samia Ahueni kwa Waliokwama NIDA
Na Thomas W. Nyakabengwe-NIDA
Kumekuwa na maombi mbalimbali ya mabadiliko ya taarifa za watu ambayo yamewasilishwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kipindi kirefu, lakini hayakuweza kufanyiwa kazi, kutokana na kutokidhi matakwa ya kisheria na utaratibu wa usajili.
Kati ya maombi ambayo hayakufanyiwa kazi ni ya waathirika wa vyeti vya kughushi, waliofukuzwa katika ajira za Serikali kutokana na kutumia vyeti vya shule vya kughushi ambapo pia walitumia vyeti hivyo kujisajili NIDA.
Maombi mengine ni ya watu waliotumia majina ya watu wengine kupata vyeti vya elimu, waliotoa taarifa za uongo/udanganyifu katika usajili wa NIDA na raia wa Tanzania waliojisajili kama Wakimbizi.
Hali hiyo ilileta mkwamo na taharuki kwa wananchi hao kupata huduma mbalimbali kama afya, fedha, biashara, elimu, mafao, ajira na usafiri kwa kuzitaja chache kwa sababu takriban huduma zote zinahitaji utambulisho wa utaifa.
Ni dhahiri kwamba malalamiko mengi yalielekezwa NIDA kwamba imekuwa kikwazo kwa wananchi hao kupata ajira, elimu kusafiri nje ya nchi, bima ya afya, mafao, pensheni, mikopo kwa ajili ya mitaji kutoka kwenye taasisi za fedha kwa sababu kulikuwa na kukinzana kwa taarifa zilizomo kweye mfumo wa NIDA na nyaraka zao nyingine.
Kufuatia hali hiyo, Serikali Sikivu ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwenye Falsafa ya 4R ambazo ni Reconciliation” yaani Maridhiano au Upatanisho, “Resilience” Ustahimilivu, “Reforms” Mageuzi na “Rebuild” ikimaanisha Kujenga Upya. Serikali imeamua kutumia R ya kwanza ambayo ni Maridhiano au Upatanisho ili kutatua tatizo hilo.
Upatanisho huu kati ya NIDA na wananchi, unatokana na uamuzi wa Serikali kutoa kibali maalum kwa ajili ya kushughulikia maombi hayo ya mabadiliko ya taarifa ambayo awali hayakuweza kufanyika kutokana na kukinzana na miongozo inayosimamia mabadiliko ya taarifa.
Serikali imepeleka tabasamu kwa waathirika ambao baadhi imewachukua miaka kadhaa bila mafanikio kwa sababu miongozo hairuhusu. Hata hivyo, kibali hicho maalum, kimetolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Oktoba 2025 na zoezi hili litafungwa baada ya muda huo kuisha.
Hapa busara imetumika zaidi na kuweka sheria pembeni kidogo kwa mwaka mmoja ili Watanzania watoe taarifa sahihi na kweli na kuweka rekodi zao sawa kwenye mfumo wa NIDA, na kunufaika na huduma za utambuzi na usajili.
Hakika busara na hekima vimetumika kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu, waombaji hao walitakiwa kufikishwa kwenye mkono wa Sheria ili Sheria ichukue mkondo wake kwa sababu walifanya udanganyifu.
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji aliwatoa hofu waombaji kwamba huo sio mtego wa kuwakamata waliotoa taarifa za udanganyifu wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari Novemba 27, 2025, Makao Makuu ya NIDA, jijini Dar es Salaam.
Hivyo, wenye changamoto hiyo wajitokeze kwenye Ofisi za NIDA za Wilaya kwa wakati uliopangwa kwa sababu alisema muda hautaongezwa.

