Rais Dkt. Samia Atoa Msamaha kwa Waliotoa Taarifa Zisizo Sahihi NIDA
Na: Alphani Mlacha
Serikali imetoa kibali maalum cha mwaka mmoja cha kushughulikia maombi ya mabadiliko ya taarifa ambayo hayakuweza kufanyika kutokana na kukinzana na miongozo ya mabadiliko ya taarifa.
Kibali hicho kilichotolewa kuanzia Oktoba 2025, kinahusisha waathirika wa vyeti vya kughushi, waliofukuzwa katika ajira za Serikali kutokana na kutumia vyeti vya shule vya kughushi ambapo pia walitumia vyeti hivyo kujisajili NIDA.
Kundi jingine ni la watu waliotumia majina ya watu wengine kupata vyeti vya elimu, waliotoa taarifa za uongo/udanganyifu katika usajili wa NIDA na raia wa Tanzania waliojisajili kama Wakimbizi.
Msamaha huo umetangazwa na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji katika Mkutano wa Waandishi wa Habari, uliofanyika Makao Makuu ya NIDA, Jijini Dar es Salaam, Novemba 27, 2025.
“Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa kibali maalumu cha marekebisho ya taarifa kwa waathirika wa vyeti vya kughushi, waliofanya udanganyifu wakati wa kujisajili katika taarifa za NIDA pamoja na raia waliojiandikisha kama wakimbizi kwa udanganyifu’’ alisema.
Aliwasihi waombaji kutumia vyema fursa hiyo kwa sababu muda uliotengwa utakapoisha hautaongezwa. Huduma hiyo itatolewa katika Ofisi za Usajili za NIDA zilizopo kila Wilaya na kuwakumbusha kwenda wakiwa na viambatisho pamoja na nakala ya vyeti vya elimu, cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), hati ya kubadili majina ‘Deed pool’ iliyosajiliwa na Gazeti la Serikali na nyaraka nyingine zitakazohitajika na Afisa Usajili wa Wilaya.
Alisisitiza waombaji wa vitambulisho kutoa taarifa sahihi na za kweli wanapofika katika ofisi za NIDA wakati wa usajili ili kujiepusha na marekebisho ya taarifa yasiyo ya lazima ya mara kwa mara.

