emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe


MKURUGENZI MKUU NIDA AWATAKA WATUMISHI KUZINGATIA NIDHAMU NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA UMMA

Na. Calvin Minja

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) James Kaji, amewataka watumishi wa NIDA kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, sheria na kanuni za utumishi wa umma.

Amesema hatavumilia mtumishi yeyote atakayekiuka misingi ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yake. Amesisitiza umuhimu wa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika maeneo yote ya kazi.

“Sitavumilia mtumishi yeyote atakayekiuka misingi ya utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yake. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunazingatia taratibu, nidhamu na uwajibikaji katika kazi,” amesema Kaji.

Ameyasema hayo leo wakati wa kikao kazi na watumishi wa NIDA mkoa wa Kagera kilichofanyika katika ukumbi wa ELCT Bukoba Hotel, Kagera.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Fedha na Utawala NIDA, George Seni, amehimiza umuhimu wa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia misingi yote ya utumishi wa umma.

“Tujitume kwa bidii, tuwe waaminifu na tufuate taratibu zote za utumishi wa umma. Ufanisi wa NIDA unatokana na juhudi za kila mmoja wetu katika kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Seni.

Aidha, viongozi hao wamewahimiza watumishi kuendelea kushirikiana, kuwa wabunifu na kuhakikisha huduma za NIDA zinatolewa kwa weledi na kwa wakati ili kuongeza ufanisi na imani ya wananchi kwa Mamlaka.