WANANCHI KUFUATILIA MREJESHO WA MAOMBI YA NIDA KUPITIA SMS
Mwananchi aliyesajiliwa kwa ajili ya kupata Kitambulisho cha Taifa anaweza kufuatilia ili kujua kama Kitambulisho chake kimekwisha kutoka au bado kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwenda katika namba maalum na hatimaye kupata majibu yake papo hapo.
Huduma hii mpya ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa - NIDA inatarajiwa kuzinduliwa wakati wowote kuanzia sasa na inalenga kumuondolea usumbufu mwananchi wa kufika katika ofisi za NIDA wilayani kufuata huduma hiyo au kupiga simu katika Kituo cha Huduma kwa Mteja badala yake yeyé mwenyewe kufuatilia maombi yake kupitia simu yake.
Ili kufahamu kama Kitambulisho kimechapishwa mwananchi atatakiwa kuandika na kutuma Namba sahihi ya Utambulisho wake wa Taifa (NIN) kwenda Namba.15274 kisha atapokea majibu kupitia simu yake ya kiganjani, kumfahamisha kama Kimechapishwa au hatua ambayo maombi yake ya Utambulisho wa Taifa, yamefikia.
Kwa mwananchi anayetaka kujua kama Namba yake ya Utambulisho wa Taifa imetoka anatakiwa kuandika Namba yake ya usajili (ERN) ikifuatiwa na jina la kwanza la mwombaji*jina la mwisho la Mwombaji*tarehe, mwezi na mwaka wa kuzaliwa mwombaji*jina la kwanza la Mama*Jina la mwisho la Mama. Mfano (MUSA*JUMA*02031987*MARIAM*ALI) kisha kutuma kwenda Namba. 15274 na atapokea ujumbe papo hapo kumjulisha Namba yake ya Utambulisho wa Taifa na kama bado itamjulisha hatua ambayo maombi yake yamefikia.
Wananchi wanaombwa kutumia fursa hii kwa kutuma SMS kwenda Na. 15274 na kutumia huduma nyingine za kupata mrejesho zilizowekwa na NIDA ikiwa ni pamoja na kupiga simu Namba 0232210500 katika Kituo cha Huduma kwa Mteja na kupitia tovuti ya NIDA www.nida.go.tz ili kupata mrejesho wa kufahamu maendeleo ya hatua taarifa zao za Usajili zilipofikia.

