
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA afanya kikao kazi na watumishi wa Kanda ya Kusini
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA afanya kikao kazi na watumishi wa Kanda ya Kusini
Na. Calvin Minja
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, amefanya kikao kazi na maafisa wa NIDA wa Kanda ya Kusini kilichohusisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Kikao kazi hicho na mafunzo Septemba 6 na 7, 2025, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, mkoani Mtwara.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaji aliwataka watumishi wa NIDA kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, huku akisisitiza umuhimu wa kuwahudumia wananchi kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyotarajiwa. Amesema wananchi wanapaswa kuona tofauti kupitia huduma zinazotolewa na NIDA na hilo linawezekana iwapo kila mtumishi atatimiza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Ndugu George Seni, aliwataka watumishi wote kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na miongozo ya kiutendaji. Aliongeza kuwa nidhamu ya kazi na uwajibikaji ni msingi wa taasisi kufanikisha malengo yake.
Aidha, kikao hicho kiliambatana na mafunzo maalum kwa watumishi kuhusu VVU/UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY). Wataalamu waliotoa mada waliwashauri watumishi kutunza afya zao kwa kufanya mazoezi, kula mlo kamili na kupima afya mara kwa mara ili kujua mwenendo wa afya zao. Watalamu walisisitiza msingi wa utendaji kazi bora ni kuwa na afya njema, hivyo kila mtumishi anapaswa kuipa afya kipaumbele.
Kikao kazi na mafunzo hayo yameelezwa kuwa fursa muhimu ya kubadilishana mawazo, kuimarisha mshikamano wa kikazi pamoja na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa NIDA katika kuwahudumia wananchi wa Kanda ya Kusini na Tanzania kwa ujumla.