
WATUMISHI WAHIMIZWA KUBADILI MTINDO WA MAISHA ILI KUJIKINGA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
WATUMISHI WAHIMIZWA KUBADILI MTINDO WA MAISHA ILI KUJIKINGA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Na. Hadija Maloya – Tanga
Mtaalamu wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, Dkt. E. Magiri amewahimiza watumishi wa NIDA kuishi mtindo bora wa maisha ili kujikinga na magonjwa sugu yasiyoambukiza.
Wito huo umetolewa kwenye mafunzo yaliyotolewa kwa watumishi wa NIDA kanda ya Kaskazini Septemba 13, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Jijini Tanga.
Akitoa tafsiri ya magojwa sugu yasiyoambukiza, mtaalamu Magiri amesema kuwa ni magonjwa ambayo hayawezi kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa njia ya kuambukizana, isipokuwa huingia kwa mtu taratibu kwa muda mrefu (gradually) na hufanya uharibifu wa viungo vya mwili, kunakopelekea kushindwa kufanya kazi ipasavyo kwa viungo hivyo hatimaye kusababisha ulemavu na hata kifo.
Dkt. Magiri ameainisha aina za magonjwa hayo kwa kusema kuwa kuna magonjwa yanayoathiri moyo pamoja na mishipa ya damu, saratani, magonjwa sugu ya mapafu, kisukari, magonjwa ya viungo na misuli, magonjwa sugu ya Afya Akili, ulemavu sugu wa mishipa ya fahamu, magonjwa yanayotokana na ajali kama vile kuvunjika mifupa, kuharibika kwa Ubongo pamoja na magonjwa ya kurithi ya damu mfano Seli nundu.