emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe


SENI ASISITIZA KUTENGA MUDA WA KUPIMA AFYA

SENI ASISITIZA KUTENGA MUDA WA KUPIMA AFYA

Na. Hadija Maloya – Tanga

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, George Seni amewataka watumishi kutenga muda wa kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka.

Msisitizo huo umetolewa wakati wa kufungua mafunzo ya kuwaelimisha watumishi wa NIDA Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, kuhusu magonjwa mbalimbali yakiwemo yanayoambukiza, yasiyoambukiza na afya ya akili yaliyotolewa katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Septemba 13, 2025 Jijini Tanga.

Katika kuweka msisitizo zaidi kwa watumishi, Seni amewataka kusikiliza kwa makini mada zote zitakazowasilishwa na wataalam, ili kufahamu kiundani tafsiri, aina, chanzo, namna ya kujikinga pamoja na matibabu ya magonjwa hayo kwa yale yanayotibika.

Aidha, amesema kuwa NIDA inatoa mafunzo haya kwa kuwa inajali afya za watumishi wake, hivyo haina budi kuwapatia mafunzo yanayohusu magonjwa mbalimbali ili kuwawezesha kulinda afya zao kwa wale ambao hawajaathiriwa na magonjwa, lakini kwa ambao kwa namna moja au nyingine wameshaathiriwa na magonjwa, waweze kuchukua hatua za matibabu, ikiwemo namna bora ya kuishi na magonjwa hayo “Nitumie fursa hii kuwahimiza kupima afya kwa ridhaa yenu kwani ukijua hali ya afya yako itakuwezesha wewe kuishi kulingana na hali hiyo kama itakavyoshauriwa na wataalamu wa afya, zingatieni hilo kwa manufaa yenu, Taasisi na Taifa kwa ujumla kwa kuwa afya ndio mtaji wa kwanza” Alisema Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.

Alimalizia kwa kuwashukuru wataalamu wa Afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo kwa kuridhia na kukubali kutenga muda wao kwa ajili ya kutoa elimu, hakika elimu hiyo ya magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza, imekuwa ya manufaa makubwa kwa watumishi wa NIDA.


UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29, 2025

Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura