
NIDA yaendelea na Elimu Ofisi za Wilaya
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa NIDA, Geofrey Tengeneza akitoa Elimu kwa Umma kwa wananchi akiwa ameambatana na John Mukobo, Afisa Usajili katika Ofisi ya Usajili, wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, leo Oktoba 01, 2025, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza Kampeni za Kuhamasisha na Kuelimisha Umma zinazoendeshwa na Mamlaka hiyo kwa nyakati na maeneo tofauti.
Tengeneza, Akizungumza na wananchi hao, amewahimiza kutumia zaidi mifumo ya kielektroniki katika kupata huduma za Usajili na Utambuzi wa Watu kwani sasa NIDA, imeendelea kuboresha huduma zake kila uchao kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma takribani zote kiganjani.
Amefafanua zaidi kwa kusema kuwa kwa sasa wananchi hawana haja tena ya kufika ofisini kupanga foleni ya kuchukua fomu na kujisajili kwa hatua ya awali bali wajisajili kimtandao kupitia eonline.nida.go.tz ili kuepuka foleni isiyo ya lazima.
"Mwananchi anapojisajili Kimtandao, anakuwa ameshakamilisha 75% ya Usajili na kubakiwa na hatua ya kupita kwenye Dawati la Afisa Uhamiaji na kuchukuliwa alama za kibaikolojia kisha maombi yake kupelekwa hatua za mbele zaidi kwa haraka ili kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa(NIN) mapema ndani ya muda wa kuanzia siku 4 hadi 7 za kazi".
Sambamba na huduma hiyo, amewataka wananchi pia, kutumia mifumo ya NIDA, ya kielektroniki katika kupata mrejesho wa maendeleo ya Maombi yao ya Utambulisho wa Taifa na huduma nyingine mtambuka kuhusiana na Usajili na Utambuzi wa watu.
"Mwananchi sasa anaweza kufahamu iwapo NIN ama Kitambulisho chake Kimeshachapishwa kwa kutuma Namba yake ya Usajili(ERN) au ya Utambulisho wa Taifa (NIN) kupitia kutuma SMS kwenda Na. 15274 kutaja baadhi"
Kwa upande mwingine wa kampeni yake ya Uhamasishaji, amepata pia wasaa wa kuendelea kuwaelimisha watumishi huku akiwakumbusha kuendeleza utamaduni mzuri ambao Mamlaka imekuwa nao wa kutoa huduma bora kwa wateja kwa kuzingatia maadili yanayoongoza mahali pa kazi ikijumuisha pia Matumizi ya Lugha ya Staha na Kutatua changamoto, kero au malalamiko ya wateja ili kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha watumishi wanatekeleza majukumu yao kwa kujali Utu baina yao na wanaowapatia huduma yaani wananchi.