Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Yaahidi Ushirikiano kwa NIDA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, imeahidi kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili iweze kutekeleza vema majukumu yake ya Usajili na Utambuzi wa watu nchini kwa kuhakikisha kila mwananchi aliyekidhi vigezo vyote vinavyotakiwa anasajiliwa na kupatiwa Utambulisho wa Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Daniel Sillo (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, wakati Kamati hiyo ilipotembelea Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na kujionea namna ambavyo taarifa za Utambuzi wa Watu zinavyopokelewa na kuchakatwa na mpaka kuchapishwa kwa Vitambulisho vya Taifa kwa waombaji wa Vitambulisho hivyo.
“Tumejionea namna mnavyofanya kazi nzuri na kwa uzalendo mkubwa, sisi Kamati tunaahidi kuwapa ushirikiano mkubwa ili muweze kutekeleza majukumu yenu ya Usaji na Utambuzi wa watu kikamilifu” amesema Mhe. Sillo
Mhe. Sillo, ameipongeza Seikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha NIDA kibajeti na kuweza kuendelea Kusajili, Kutoa Namba za Utambulisho wa Taifa na Vitambulisho kwa wananchi. Ameipongeza NIDA kwa kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa licha ya changamoto zinazoikabili Mamlaka.
Kwa upande wake Mhe. Sagini amesema kuwa toka NIDA ilipoanza kusajili na Kutambua watu mwaka 2012, imefanikiwa Kusajili na Kutambua watu nchini zaidi ya milioni 23 sawa na 77.2 ya watu 31,020,943 wenye miaka 18 na zaidi kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Imezalisha Namba za Utambulisho wa Taifa(NIN) 20,126,693 sawa na 84.0 ya watu waliosajiliwa na kuchapisha Vitambulisho vya Taifa zaidi ya milioni 12 na kati ya hivyo, milioni 10 vimesambazwa kwa wananchi.
“Jitihada zinazofanywa ni kubwa ambapo kwa kuwezeshwa na Serikali, NIDA wamepokea kadi ghafi kwa ajili ya kuchapishia Vitambulisho vya Taifa na wataendelea kupokea kadi ghafi zaidi katika mwaka ujao wa fedha jambo litakalowezesha wananchi ambao hawajapata Vitambulisho vyao vya Taifa kupatiwa Vitambulisho hivyo.” Alisema Mhe. Sagini
Amebainisha kuwa wataalamu wa ndani wa ujenzi wa mifumo wa NIDA wamefanikiwa kujenga na kusimika jumla ya mifumo ishirini na tatu (23) kati ya 42 iliyokusudiwa na hivyo Serikali kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 4 ambazo zingetumika kwa ujenzi wa mifumo hiyo. Amesema hatua hiyo imechagizwa pia kutokana na kuwawezesha wataalamu hao kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu.
Kuhusu utanuzi wa matumizi ya taarifa za Mfumo wa Utambuzi wa Watu zinazohifadhiwa na NIDA, Mhe. Sagini, amesema kuwa NIDA imefanikiwa kuunganisha jumla ya wadau 75 ambapo miongoni mwa hizo 34 ni wa Taasisi za Serikali na binafsi ni 41. Amesema hatua hii imeiwezesha NDA kukusanya maduhuli ya zaidi ya Shilingi Bilioni 4 hadi kufikia Juni, kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefanya marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Usajili na Utambui wa Watu za mwaka 2014 kwa kuondoa ukomo wa muda wa matumizi ya vitambulisho kwa raia hivyo kuwezesha kuendelea kutumika katika kupata huduma za kijamii na kiuchumi. Aidha imefanya pia marekebisho katika huduma ya Ushirikishanaji Taarifa, Usajili wa Walowezi na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora).