emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe


Rais Samia: Tutumie Namba Moja Tu ya Mtanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Kassim kwa kushirikiana na Wizara kuhakikisha taarifa zote za Mtanzania zinapatikana kwenye Namba ya NIDA ili kuondokana na udanganyifu na usumbufu wa kupata huduma kwenye taasisi mbalimbali.
Ameyasema hayo alipokua akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Baharini (Submarine Cable) wa 2Afrika na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kasi ya 5G ya Airtel iliyofanyika Tanki Bovu – Dar es Salaam.

Sambamba na hilo Waziri Mkuu ameelekezwa kusimamia na kuhakikisha kuwa mtoto anapozaliwa anapatiwa NIN kwa kutumia cheti anachopewa hospitali Ili atambulike na hii itasaidi kumtambua mtoto kazaliwa wapi, jinsia yake, uzito aliozaliwa nao na afya yake kiujumla ambapo itarahisisha taasisi nyingine kupata taarifa hizo kupitia Namba ya NIDA.

Katika kutekeleza hilo, Mhe. Rais amewataka Watanzania wote kuhakikisha taarifa ambazo wamezitoa NIDA ni sahihi na kama zina makosa ni vyema zikafanyiwa mabadiliko kulingana na taratibu na miongozo iliyopo ili kujuana nani ni nani, mwenyeji wa Tanzania ajulikane na mgeni pia ajulikane.

“Nitoe wito kwa kila Mtanzania ahakikishe kuwa taarifa alizotoa NIDA ni sahihi, kama siyo sahihi aende akarekebishe ili atambulike kwa taarifa hizo alizotoa na taasisi zote zinazotoa huduma kwa Watanzania kutumia Namba ya NIDA kuweza kujuana NANI NI NANI ndani ya nchi yetu”

Ifahamike kuwa Kitambulisho cha Taifa kina uwezo wa kubeba taarifa mbalimbali kama za benki, bima ya afya, leseni ya udereva na taarifa nyinginezo. Na hii itasaidia kuondoa usumbufu kwa Wananchi katika kupata huduma lakini pia kuondoa usumbufu wa Mtanzania kutembea na kadi zaidi ya moja.

Kwasasa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inafanya kazi na taasisi za umma na binafsi kwa kuzisaidia kuwatambua wateja wao hali inayoongeza ufanisi katika utoaji wa huduma zao na kufanya huduma imfikie mhusika kimahsusi, kwa haraka na kwa usalama zaidi.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inawasisitizia wananchi wote kuandikisha taarifa sahihi kwa ambao taarifa zao zina makosa wanashauriwa kufika katika Ofisi za NIDA za Wilaya kwa ajili ya kufanya marekebisho ya taarifa hizo mapema iwezekanavyo kabla ya kupatwa na dharura.