emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe


Mafanikio ya NIDA Katika Miaka 3 ya Srikali ya Awamu ya Sita

Unapozungumzia suala la Usajili na Utambuzi wa Watu Nchini bila shaka utakuwa pia unaizungumzia Taasisi ya Mamalaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambayo ndiyo yenye jukumu kuu la kusimamia suala la Usajili na Utambuzi wa watu pamoja na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi, wageni wakaazi pamoja na wakimbizi halali wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.

NIDA ilianza rasmi shughuli za Utambuzi na Usajili wa watu nchini Mwaka 2012 ambapo pamoja na changamoto za hapa na pale inayo mengi ya kujivunia.

Leo hii Serikali ya awamu ya sita (6) chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inapofikisha kipindi cha miaka 3 yaani katika hatamu za kuiongoza nchi yetu kuanzia Machi, 2021 – Januari, 2024, NIDA imepata mafanikio kadhaa ya kujivunia. Katika kipindi hicho cha awamu hii ya sita, NIDA imeendelea kuimarisha na kutekeleza shughuli za Usajili na Utambuzi wa watu nchini kote Tanzania Bara na Zanzibar kupitia ofisi za Usajili za Wilaya ili kuhakikisha watu wote wenye vigezo wanasajiliwa na kutambuliwa. Jumla ya wananchi 2,442,744 wamesajiliwa katika kipindi hicho hivyo, kufikisha jumla ya wananchi 24,495,804 waliosajiliwa na kutambuliwa hadi Januari, 2024 toka kuanza kwa usajaili na utambuzi wa watu mwaka 2012. Vivyo hivyo katika kipindi hicho cha miaka mitatu, jumla ya Namba za Utambulisho wa Taifa (NINs) 2,003,256 zimezalishwa na hivyo kufanya Namba zilizokwisha kutolewa kuwa 20,768,171.

Kuhusu uzalishaji na ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi, tatizo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu,  Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa  katika kuondokana na tatizo hilo ilikuja na mpango mkakati wa  uzalishaji mkubwa wa vitambulisho vya Taifa (Mass production) sambamba na ugawaji wa Vitambulisho kwa Umma (mass issuance) ulioaza kutekelezwa mwezi Oktoba 2023.

Msemaji wa NIDA Geofrey Tengeneza amesema kuwa uzalishaji huo mkubwa ni matokeo ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuiwezesha NIDA kupata fedha hususani fedha kwa ajili ya kununua kadighafi kiasi cha Shilingi 51,500,000,000.00 na kuweza kufanikisha kununua kadighafi 13,514,251 ambapo hadi Januari, 2024 kadighafi zote zimekwishapokelewa kutoka kwa Mkandarasi na kazi ya uzalishaji vitambulisho ikaanza kwa kasi kubwa na inatarajiwa hadi Machi, 2024 wananchi wote waliosajiliwa na kupatiwa Namba za Utambulisho (NINs) watakuwa wamepatiwa vitambulisho vyao vya Taifa.

Amesema tayari katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt Samia madarakani vitambulisho 12,561,983 vimezalishwa na vitambulisho 10,245,650 vimesambazwa na kugawiwa kwa wananchi. Idadi hii inafanya jumla ya vitambulisho vya Taifa vilivyokwisha kuzalishwa kufikia 19,593,384 na Vitambulisho vilivyokwisha kusambazwa kwa wananchi kufikia 17,161,600. Zoezi la uzalishaji, usambaji na ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa katika ofisi za serikali za mitaa, vijiji, vitongoji na shehia ambako ndiko tunapeleka vitambulisho hivyo kwa wananchi kuvichukua linaendelea. Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeiwezesha NIDA kumaliza tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi.

Kuhusu uunganishaji wa ofisi za Wilaya Tengeneza amesema kuwaKatika kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi Januari 2024, ofisi za usajili za wilaya ishirini na mbili (22) zimeunganishwa na kituo cha uchakataji wa Taarifa na kufanya jumla ya ofisi za usajili zilizounganishwa na kituo hicho kote nchini kuwa 153.

 “Lengo ni kuwezesha mawasiliano kati ya ofisi za usajili na kituo cha uchakataji taarifa, na kuhakikisha maombi ya watu wote waliosajiliwa yanasafirishwa kutoka Ofisi za Usajili za Wilaya kwenda Kituo cha Kuchakata taarifa (Data center) kwa ajili ya uchakataji na uzalishaji vitambulisho kwa wakati” amesema.

Aidha, Mamlaka ya Vitambulisho imefanikiwa kuunganisha mfumo wake na taasisi nyingine kadhaa ambapo katika kipindi hicho cha miaka mitatu jumla ya taasisi 40 za Umma na Binafsi zimeunganishwa katika mfumo wa Usajili na Utambuzi wa watu na hivyo kufikia jumla ya Taasisi 96 zilizounganishwa mpaka sasa. Lengo la hatua hii  ni kurahisha utoaji huduma na utambuzi wa wananchi wanaopata huduma katika Taasisi hizo. Hivyo, watu wote wenye utambulisho wa Taifa (NIN) wanaweza kupata huduma zote wanazostahili nchini.

Eneo jingine ambalo NIDA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ni kuweza kukusanya jumla ya Shilingi 52,563,367,267.78 kwa kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi Januari, 2024 na hivyo, kuongeza wigo wa makusanyo ya fedha za Serikali. Mafanikio haya yanayotokana na NIDA kuwa na Kanzidata yenye taarifa za watu. Aidha, fedha hizo zimewasilishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

“Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita (6) chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan NIDA imefanikiwa kukusanya maduhuli ya Serikali ya shilingi Bilioni 52.5 na kutunukiwa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tuzo ya mshindi wa tatu miongoni mwa taasisi na Mashirika ya Serikali yasiyo ya Kibiashara  yaliofanya vizuri zaidi katika kuchangia Mfuko  Mkuu wa Serikali hadi kufikia juni 2023” amesema Msemaji wa NIDA Geofrey Tengeneza.

Kwa upande wake Mkurugenzi  wa Idara ya Uzalishaji Vitambulisho wa NIDA Edson Guyai anasema pamoja na hayo yote Mamlaka katika kipindi cha utawala wa Serikali ya awamu ya sita Mamlaka imefanikiwa pia kuboresha huduma ya usajili na utambuzi kwa kuanzisha huduma ya usajili mtandaoni (online registration). Mfumo huu umeanza kutumika mwaka 2022/2023 na umeonesha ufanisi huku ukisaidia kupunguza uhitaji wa usajili kufanyiwa ofisini.

“Huduma hii inamwezesha mwananchi kujisali kwa njia mtandao mahali popote alipo ndani na nje ya nchi na inalenga kumuondolea mwananchi usumbufu wa kwenda katika ofisi zetu za usajili za Wilaya” amesema.

Guyai amesema kuwa kwa mara ya kwanza NIDA imefanikiwa pia kusajili watanzania wanaoishi nchi za nje ambao bado hawajakana uraia wao wanaojulikana kama (Diaspora). Usajili huu wa majaribio ulifanyika katika nchi za Marekani, Uingereza na Uholanzi. Hii ni hatua kubwa ikiwa ni katika kuunga juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan baada ya maombi ya Diaspora ya kusajiliwa ili waweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi nchini