NIDA Yangara kwenye Maonesho ya Biashara na Utalii – Tanga, 2024
Na.Calvin Minja – NIDA
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA imeibuka Mshindi wa Kwanza kwa taasisi za umma zilizotoa huduma kwenye Maonesho ya 11 ya Biashara na Utalii yaTanga yalifanyika Mei 28 hadi Juni 6, 2024.
Hafla ya kufunga maonesho hayo imefanyika Juni 06, 2024, kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi. Batilda Salha Burian ambapo NIDA ilitangazwa kuwa mshindi wa kwanza katika kutoa Huduma Bora kwa Wananchi kati ya taasisi za umma zilizoshiriki na kutoa huduma kwenye maonesho hayo ikifuatiwa na mshindi w pili BRELLA na TANESCO kuibuka mshindi wa tatu.
Balozi, Dkt. Burian ameipongeza NIDA kwa kuibuka Mshindi wa Kwanza, lakini pia ameitaka kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
“NIDA wamesogeza huduma zao karibu na wananchi katika maonesho haya na kutatua changamoto mbalimbali zilizowakabili.” alisema Balozi, Dk. Burian. Kwa upande wake Afisa Usajili NIDA Mkoa wa Tanga, Hawa Hamadi akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, NIDA ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi kwani jukumu la kuwahudumia wananchi kuhakikisha wanasajiliwa, wanatambuliwa na kutambulishwa.
“Ni furaha kwetu NIDA, kuibuka kinara miongoni mwa taasisi zote za Serikali zilizoshiriki katika maonesho hayo yaliyokuwa na jumla ya washiriki 195 wa kitaifa na kimataifa, hili ni deni kwetu kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kama ilivyo ahadi yetu.
Huduma zetu hazitaishia hapa, tunawakaribisha wananchi wote kwenye Ofisi zetu za Mkoa zilizoko Chuda, wananchi wote wanakaribishwa kwa ajili ya usajili, na maulizo mbalimbali. Ofisi zetu zipo wazi siku za kazi kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri.” alisema Hawa.
Naye Agnes Gerald, Afisa Habari Mwandamizi wa NIDA akimwakilisha Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, alisema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza maelekezo na matakwa Serikali ya Awamu ya Sita na kuhakikisha azma ya kutoa huduma bora kwa wananchi wote inaendelea kutekelezwa kwa vitendo, sanjari na kuendelea kuhamasisha umma kwa kushirikiana na uongozi, wa mikoa hadi ngazi ya serikali za mitaa, vyombo vya habari, viongozi wa dini na wadau wengine ili wananchi waendelee kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao vya taifa katika Serikali zao za Mitaa kwa kuwa NIDA imevichapisha kwa wingi na kuvisambaza huko.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi, Dkt. Batilda Buriani, ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi, akiitunuku NIDA, Tuzo na Cheti cha Ushindi, kutokana na kuibuka Mshindi wa Kwanza katika kutoa Huduma Bora kwa Wateja, miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizoshiriki kwenye Maonesho ya 11 ya Biashara na Utalii ya Tanga, yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, mkoani Tanga, kuanzia tarehe 28 Mei – 06 Juni, 2024. Kulia ni Hawa Maulidi, Afisa Usajili wa Ofisi ya Usajili ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mkoani Tanga, katikati ni Agnes Gerald, Afisa Habari Mwandamizi kutoka NIDA
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi, Dkt. Batilda Buriani, ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi, akipatiwa maelezo ya huduma zinazotolewa kwenye banda la NIDA, na Agnes Gerald, Afisa Habari Mwandamizi kutoka NIDA, kwenye Maonesho ya 11 ya Biashara na Utalii ya Tanga, yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, mkoani Tanga, kuanzia tarehe 28 Mei – 06 Juni, 2024. Kushoto ni Hawa Maulidi, Afisa Usajili wa Ofisi ya Usajili ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mkoani Tanga,