NIDA Yawa Ufunguo wa Maendeleo Nchini Tanzania
Na: Agnes Gerald – NIDA
Suala la kutambua watu kielektroniki katika dunia ya leo haliepukiki kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoshika kasi na kuifanya dunia kuwa kama kijiji.
Jambo hili linaleta ulazima kwa nchi mbalimbali kuanzisha mifumo ya kusajili na kutambua watu kielektroniki, sambamba na mifumo hiyo kuwa na uwezo wa kushirikishana taarifa kitaifa na kimataifa ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao na taifa kwa ujumla.
Kutokana na uhitaji huo usioepukika kitaifa na kimataifa ndipo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) iliyo miongoni mwa taasisi za Muungano chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ilipotimu 2008 ikaanzishwa chini ya Hati ya Uanzishwaji wa Mamlaka ya mwaka 2008 (Establishment Instrument, 2008) GN 122/2008 na kukasimishwa majukumu kadhaa ikiwa ni pamoja na kusajili na kutambua watu wanaoishi nchini, kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia, wageni waakazi na wakimbizi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kujenga utawala bora wa mamlaka, kutunza Daftari Kuu la Kielektroniki la Taifa la Usajili na Utambuzi wa Watu hapa nchini na kushirikisha taarifa zilizoko kwenye daftari hilo wadau wengine.
Ushirikishaji wa daftari hilo unalenga kuwawezesha wadau kuwatambua wateja wao kimahsusi, kwa uhakika njia ambayo ni salama zaidi, ya haraka na gharama nafuu sanjari na kuwawezesha wananchi kupatiwa huduma kirahisi zaidi ikilinganishwa na awali na kuepukana na adha ya kubeba vitambulisho lukuki.
Ameyasema hayo Geofrey Tengeneza, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, NIDA alipokuwa akiuhabarisha umma juu ya mafanikio NIDA iliyoyapata tangu kuanzishwa kwake 2008 takribani miaka16 iliyopita. Tengeneza anasema NIDA inafanya kazi zake kwa kutekeleza sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu ya mwaka 1986 na marejeo ya mwaka 2012 [CAP 36 R.E 2012] na Kanuni za Usajili na Utambuzi za Mwaka 2014.
“Makala haya yamelenga kukujuza si tu majukumu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, bali pia mafanikio na changamoto zilizojitokeza pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008”.
Akiweka wazi mafanikio ambayo Mamlaka imeyafikia tangu kuanzishwa kwake anasemaNIDA, ilianzishwa (Mwaka 2008) baada ya Muungano na imefanikiwa kutekeleza mengi ikiwemo kukua na kuimarika zaidi kimuundo kwani ilipoanzishwa ilikuwa ina idara nne (4) ambazo ni ID Management, Management Information System, Business Support Services, na Ofisi ya Zanzibar na vitengo vitatu (3) ambavyo ni: Ukaguzi wa Ndani (Internal Audit Unit), Manunuzi (Procurement Management Unit), na Huduma za Sheria (Legal Services Unit).
Tunapoadhimisha Miaka 60 ya Muungano, muundo wa NIDA umebadilika na sasa kuna idara sita (6) ambazo ni: ID Management, Management Information System, Legal Services, Finance & Administrations, Planning & Budget na Zanzibar Coordination Office na vitengo vimeongezeka na kufikia vitano (5) ambavyo ni Uratibu wa Wilaya, Usimamizi wa Vihatarishi, Mawasiliano na Hifadhi Hati, Ukaguzi wa Ndani pamoja na Kitengo cha Manunuzi.
Mbali na hatua ya kimuundo Tengeneza, anasema, suala la Usajili na Utambuzi wa Watu nchini ndilo jukumu kuu la NIDA,ilianza usajili na utambuzi wa watu mwaka 2012 na katika kipindi cha 2012 hadi Februari, 2024 imefanikiwa kusajili jumla ya watu 24,495,804, sawa na asilimia 79 ya watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kulingana na idadi ya watu iliyokadiriwa kuwa 31,477,938 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Matokeo ya Usajili huo yamewezesha uzalishaji wa Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) 20,832,225 kiasi ambacho ni sawa na asilimia 85 ya watu waliosajiliwa na kutambuliwa. Sanjari na kuzalisha vitambulisho 20,286,420 sawa na asilimia 97.4 ya NIN zilizotolewa kwa wananchi na wageni wakaazi.
Mafanikio hayo ya kishindo yameiwezesha NIN kuondokana na tatizo sugu la upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa lililokuwa likilalamikiwa na wananchi wengi. Katika kuhakikisha kuwa tunapoadhimisha Miaka 60 ya Muungano tatizo hili linakwisha na kubaki historia, NIDA ilikuja na mpango mkakati wa kuchapisha vitambulisho vya Taifa kwa wingi (National ID Mass Production) sambamba na kugwa vitambulisho kwa umma kwa mkupuo ulioanza kutekelezwa Oktoba 2023. Zoezi hili la uzalishaji, usambaji na ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa umma linaendelea katika ofisi za serikali za mitaa, vijiji, vitongoji na shehia ambako ndiko vitambulisho vinapelekwa kwa ajili ya wananchi kuvichukua.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeiwezesha NIDA kumaliza tatizo hili la muda mrefu la upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi kwa kuipatia fedha za kununua kadi ghafi”.
Kuhusiana na suala la ujenzi wa Mifumo ya Usajili na Utambuzi wa Watu, anaeleza kuwa ni jambo la msingi ambalo NIDA imelifanyaili kufanikisha mkakati wake wa kujitegemea kimfumo na kuimarisha mfumo wa Vitambulisho vya Taifa. Mamlaka kwa kutumia wataalamu wa ndani, imefanikiwa kujenga mifumo ishirini na minne (24) kati ya mifumo 42 inayokusudiwa kujengwa. Mifumo hii imesaidia kuondokana na utegemezi wa wakandarasi kutoka nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha za Serikali.
Ameeleza faida nyingine zaidi ya kujitegemea katika ujenzi wa mifumo ni pamoja na kuondokana na ukomo wa leseni ya matumizi ya mifumo ya wakandarasi wa nje, msaada wa kiufundi kutolewa na wataalamu wa ndani, kumiliki nakala halisi ya programu za mfumo wa Vitambulisho vya Taifa na kuweza kufanya maboresho ya mfumo pindi yanapohitajika ikiwemo kuimarisha uwezo wa kutoa huduma bora kwa wadau mbalimbali.
Anasema NIDA imefanikisha Kujenga na Kutunza Daftari Kuu la Taifa la Usajili na Utambuzi wa Watu hapa nchini na kushirikisha taarifa hizo na wadau wengine takribani taasisi tisini na sita (96) za umma na binafsi (zikiwemo tatu za Zanzibar) lengo hasa ni kurahisisha uhakiki na utambuzi wa watu wanaopata huduma katika taasisi hizo, utoaji huduma kwa watu kwa urahisi, haraka na kwa usalama zaidi.
Akibainisha baadhi ya mafanikio yatokanayo na matumizi ya Daftari la Usajili na Utambuzi wa Watu ni ikiwemo kufanikisha usajili wa laini za simu, usajili wa kampuni, utoaji wa namba za walipa kodi (TIN), kudhibiti matumizi ya bima kwa wasio walengwa, kurahisisha ufunguaji wa akaunti za benki utoaji wa hati za kusafiria na utoaji wa hati za viwanja. Mafanikio mengine ni kusaidia katika kupambana na ugaidi na utakatishaji wa fedha, kupambana na makosa ya kimtandao, miamala ya fedha na ya ulinzi wa taarifa binafsi sambamba na kudhibiti uhalifu nchini kwa ujumla wake.
Ujenzi wa Kituo cha Kuhifadhi taarifa za watu (Data Centre) na Kituo cha Uokozi (Data Recovery Centre)ni miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa na NIDA. Uwepo wa vituo hivi ni jambo linalowahakikishia wasajiliwa na wadau uhakika wa taarifa zao zinavyohifadhiwa kimadhubuti na kupatikana hata pindi majanga yakitukia kama vile moto, mafuriko au matetemeko.
Katika kuhakikisha inasogeza huduma karibu kwa wananchi, NIDA imefungua Ofisi za Usajili na Utambuzi wa Watu kwenye kila Wilaya Tanzania Bara na Zanzibar Ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi wote, ambapo hadi Februari 2024 Mamlaka imefikisha jumla ya ofisi 153 na kuziunganisha kielektroniki na Kituo cha cha Kanzidata.
Mafanikio hayo yametokana na kuwepo kwa Mkongo wa Taifa unaorahisisha kufanyika kwa maunganisho hayo. Lengo ni kuhakikisha maombi ya watu wote waliosajiliwa katika Ofisi za Usajili za Wilaya Tanzania Bara na Zanzibar yanafikishwa Kituo cha Kuchakata Taarifa (Data Centre) kwa ajili ya kuchakatwa na kuzalisha vitambulisho kwa wakati.
Ili kukabiliana na changamoto ya foleni kwenye ofisi za Usajili, Mamlaka imeboresha njia za utoaji huduma kwa kuanzisha huduma ya Usajili Mtandaoni (Online Registration) ambapo mteja akijisajili anakuwa mefanya 75% ya usajili, mfumo huu unapatikana kupitia kiunganishi eonline.nida.go.tz na uko hewani tangu tarehe 21 Desemba, 2022. Hadi kufikia Februari 2024 watu 27,973 wameshajisajili, kati ya hao raia ni 25,845 na wageni wakaazi ni 2,128.
Kundi la watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) nalo lilifikiwa katika kipindi hiki, Mamlaka imefanikiwa kuwasajili watanzania 284 wanaoishi nchini Marekani, Uingereza na Uholanzi. Usajili huu wa majaribio ulifanyika katika nchi hizo tajwa, ikumbukwe hii ni hatua kubwa ikiwa ni katika kuunga juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan baada ya Diaspora kuwasilisha maombi ya hitaji la wao kusajiliwa ili waweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi nchini, zinazochochea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Yote hayo yameweza kufikiwa kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuiwezesha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kirasilimali, Tengeneza, amehitimisha kwa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu kwa kuiwezesha Mamlaka hiyo kwa kuipatia rasilimali ambazo zimetumika kuondoa tatizo sugu la upatikanaji wa vitambulisho hivyo kuleta mafanikio yaliyoonyeshwa dhahiri kwa wananchi kutambuliwa na kumiliki vitambulisho vyao.