Usajili wapamba moto Arusha; Wananchi wahamasika kujisajili

Katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa mkoa wa Arusha wamefurika kwenye vituo vya Usajili kujisajili Vitambulisho vya Taifa, zoezi ambalo limeanza tangu ijumaa wiki iliyopita.

Wakazi hao wameonyesha furaha, tofauti na matarajio ya wengi ya uchovu na manung’uniko ya kukaa foleni kwa muda mrefu. Cha kufurahisha zaidi ni utaratibu waliojiwekea wenyewe wa kujipanga foleni huku wazee, wajawazito na mama wenye watoto wachanga wakipewa kipaumbele; tabia ambayo ni kinyume na historia ya muda mrefu ya mkoa huo katika kushiriki mazoezi ya Kitaifa.

Hata hivyo wameomba uongozi wa Mamlaka kuangalia namna inavyoweza kuongeza vifaa zikiwemo mashine za Usajili ili kupunguzia wananchi adha ya kukaa foleni muda mrefu.

Kwasasa zoezi hili limeanza mkoa wa Arusha na kuhususisha Wilaya zote za Mkoa huo ambapo mpango wa usajili unakwenda kwa Kata. Kwa upande wa Kanda ya Kaskazini Mkoa mwingine ni  Kilimanjaro ambao kwa sasa uko kwenye hatua za mwisho kufanya maandalizi na zoezi rasmi la Usajili Umma litaanza Jumatano 11/10/2017 hali mkoa wa Tanga wakiwa wamekamilisha zoezi hilo na hatua ya sasa ni Uhakiki na mapingamizi pamoja na Ugawaji wa Vitambulisho.

Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Godfrey Daniel Chongolo akitoa maelekezo na taarifa ya utekelezaji zoezi la Usajili wananchi wa Longido kwa uongozi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) walipomtembelea ofisini kwake hivi Karibuni.

 

Wananchi Wilaya ya Arusha wakichukuliwa picha na mashine maalumu za Usajili wakati wa kukamilisha hatua za Usajili Vitambulisho vya Taifa.

 

Dawati maalumu la viongozi wanaohakiki Uraia na makazi ya wananchi. Kushoto ni Mtendaji wa Kata ya Themi Bw. Joackim Kisarika na kulia ni Afisa Uhamiaji mkoa wa Arusha wakiwa wamekamilisha uhakiki wa mwananchi anayeonekana kwenye picha akiweka saini kwenye rejesta.

 

Diwani wa Kata ya Themi (Chadema) Mhe. Melance Kinabo akikagua namna shughuli za Usajili Vitambulisho  vya Taifa zikiendelea katika kituo cha Nanenane. Diwani kwa kushirikiana na uongozi wa Kata wamekuwa na jukumu kubwa la kuhamasisha wananchi kushiriki kwa wingi kwenye zoezi hilo.

 

Hawa ni baadhi tu ya wananchi katika Kata ya Sombetini wakihakikiwa na kuthibitishwa uraia wao na maafisa wa uhamiaji kabla ya kuchukuliwa alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki.

 

Wananchi wa Kata ya Sombetini Arusha wakisubiri huduma kwenye zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa.

 

Wananchi wa Kata ya Sombetini Arusha wakisubiri huduma kwenye zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu