Wazo la kuanzisha Vitambulisho vya Taifa kwa raia wa Tanzania na wageni waishio nchini Tanzania lilizaliwa mwaka 1968 katika kikao cha “Interstate Intelligence Gathering” kilichojumuisha wajumbe Kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia. Kwa wakati huo nchi za Kenya na Zambia tayari zilikuwa na Vitambulisho vyao vya Taifa. Iliazimiwa kwamba ili kuimarisha mahusiano ya kiusalama yanayozingatia Utawala wa Sheria katika nchi hizo nne ni lazima nchi za Uganda na Tanzania nazo zikatoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia wao.

Kumekuwa na jitihada mbalimbali za Serikali kuhakikisha Watanzania na wageni wakazi wote wanapatiwa Vitambulisho vya Taifa, lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda yaliyotajariwa kwa kipindi kirefu kutokana na sababu mbalimbali. Mwaka 1986 Serikali ilitunga Sheria ya Vitambulisho ambayo haikutumika wala kutungiwa kanuni zake.

Ni wazi kwamba kwa wakati huu kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na Vitambulisho vya Taifa kulingana na mazingira yaliyopo. Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo nchi tano zimeungana na kukubaliana kwamba watu wa nchi hizo wanaweza kutembeleana bila bughudha pia kumeongeza umuhimu wa kuwa na Vitambulisho. Ikumbukwe kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee katika Jumuiya hiyo ambayo haina Vitambulisho vya Taifa.

Upembuzi yakinifu wa Vitambulisho vya Taifa uliofanyika mwaka 2006 umedhihirisha kuwa Mradi unatekelezeka. Aidha taarifa hiyo imeainisha makadirio ya gharama za Mradi na namna mradi utakavyotekelezwa ambapo teknolojia ya “Smartcard” ndiyo itakayotumika kama ilivyokubaliwa na Baraza la Mawaziri katika kikao kilichokaa mjini Dodoma mwezi Februari, 2007.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete tayari ametia saini Hati ya kuidhinisha kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia Vitambulisho vya Taifa kinachojulikana kama Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa au “National Identification Authority (NIDA)”. Hati hii imechapishwa katika Gazeti la Serikali, GN No.122 ya tarehe 01/08/2008.

Aidha katika Kikao chake cha tarehe 3 Februari, 2007 Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo kuwa iundwe Kamati ya Usimamizi (Steering Committee) ya Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara na Vitengo vinavyohusika na mambo muhimu kuhusu Vitambulisho vya Taifa. Kamati hii pamoja na mambo mengine itakuwa na jukumu la kutoa mwongozo na mwelekeo wa programu za Mradi.

Baraza pia liliamua kuwa taarifa ya upembuzi yakinifu ya Kampuni ya Gotham International Limited (GIL) iwe ndio mwongozo wa utekelezaji wa Mradi na Kampuni hiyo iliteuliwa kuwa Mshauri Mwelekezi wa Mradi.

Katika hatua nyingine, Serikali ilitoa mwongozo kuwa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa mradi ikiwemo ile ya mshindi wa zabuni ya mkandarasi wa kutengeneza mfumo wa Vitambulisho vya Taifa ziwasilishwe katika Baraza la Mawaziri ili kupata ridhaa yake.