HATUA MBALIMBALI ZA USAJILI NA UTAMBUZI WA WATU
Utaratibu wa Usajili na Utambuzi wa Watu unafanyika hatua kwa hatua kama ifuatavyo:
1. Ujazaji wa fomu za Utambuzi na Usajili,
2. Uhakiki wa awali wa fomu za maombi,
3. Uingizaji wa taarifa kwenye mfumo wa kompyuta,
4. kuthibitishaji taarifa za mwombaji zilizo katika mfumo wa kompyuta.
5. Uchukuaji wa alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki,
6. Utengenezaji wa Daftari Kuu la Taarifa za Watu,
7. Uhakiki wa mwisho,
8. Uchapishaji, uhakiki wa ubora na Utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
Ufafanuzi wa mambo msingi hitajika kwa baadhi ya hatua za usajili tajwa hapo juu;
1.1.1. Usajili – Ujazaji wa fomu (biographic data)
Mwombaji wa Kitambulisho Raia, Mgeni ama Mkimbizi anatakiwa kufika katika kituo/ofisi ya usajili na vivuli (Copy) ya nyaraka za kutambulisha makazi, uraia na umri wake kama ilivyoainishwa hapo juu katika kipengele cha mahitaji ya kila kundi wakati wa usajili.
1.1.2. Uchukuaji alama za kibaiolojia
Hatua hii ya Usajili inajumuisha upitiaji wa taarifa za mwombaji katika mfumo, uchukuliwaji wa alama za vidole, picha na utiaji wa saini ya kielektroniki ambapo kuna mambo msingi ya mwombaji kuzingatia ambayo ni;
- Kwa ajili ya ubora na mwonekano mzuri wa picha mwombaji unashauriwa kutovaa nguo nyeupe, pinki, kijivu, bluu mpauko au nguo zenye rangi za kungaa sana. Kutovaa kofia ya aina yoyote wakati wa kupiga picha, au kupaka hina viganjani wakati wa uchukuaji wa alama za kibaiolojia.
- Ili kurahisisha zoezi hili, mwombaji unaombwa kufika kwenye ofisi/kituo cha usajili na nyaraka halisi (original) za kuthibitisha uraia na umri wake mathalani, cheti cha kuzaliwa, pasipoti, vyeti vya elimu ya msingi na sekondari, leseni ya udereva, kitambulisho cha bima ya afya, kitambulisho cha mpigakura na kitambulisho cha mzanzibar mkazi.
1.1.3. Uhakiki na Uwekaji Pingamizi
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika hatua hii inakuwa ikiendesha zoezi la kupokea maoni ya uwekaji pingamizi kutoka kwa wananchi juu ya wakazi waliofanya maombi ya kupatiwa Vitambulisho vya Taifa na Uhakiki wa mwisho wa taarifa za waombaji kabla ya kuanza uchapaji na ugawaji wa Vitambulisho kwa wakazi ambao wamekamilisha hatua ya kuchukuliwa alama za kibaiolojia (picha, alama za vidole na saini ya kielektroniki).
NIDA kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mitaa, vyombo vya usalama na wananchi kwa jumla inakuwa ikipokea taarifa za maoni au pingamizi kuhusiana na waombaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wakazi wa maeneo husika.
Hii ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga mfumo madhubuti wenye taarifa na kumbukumbu sahihi za watu, hivyo wananchi wanaweza kutoa pingamizi la kimaandishi wakieleza sababu ya pingamizi kwa kuainisha upungufu ambao wamebaini, mathalani taarifa za URAIA, UMRI, MAJINA, PICHA na MAKAZI ya mwombaji kwa kujaza fomu maalum kwenye mtaa husika au kutoa taarifa NIDA kwa kutuandikia barua kupitia anuani S.L.P 12324 Dar es Salaam, barua pepe, au kuziwasilisha kwenye Ofisi za wilaya husika.
NIDA inawaomba wananchi kuwa wazalendo na kujitokeza kuhakiki taarifa zao na waombaji wengine, na kutoa pingamizi bila upendeleo, uonevu au kukomoana.
1.1.4. Ugawaji Vitambulisho vya Taifa
Mwombaji anatakiwa kufika katika ofisi ya usajili katika wilaya husika ama kulingana na maelekezo/matangazo yanayotolewa katika eneo hilo ili kupatiwa kitambulisho chake kwa kuzingatia kuja na risiti maalumu aliyopatiwa na NIDA wakati alipokamilisha kuchukuliwa alama za kibaiolojia.
Tufuatilie