Na. Agnes Gerald – NIDA
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu ameipongeza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kutekeleza takwa la kisheria na Tamko Na 1 la mwaka 1970 la Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere la kuwashirikisha wafanyakazi kufanya maamuzi mbalimbali kupitia baraza la wafanyakazi.
Ameyasema hayo wakati akifungua Kikao cha 26 cha Baraza la Wafanyakazi wa NIDA na kuwapongeza kwa kuwa na mada mbalimbali zinazotolewa na wataalam wabobevu wakati wa vikao vya Baraza, na kuwataka wafanyakazi kutumia elimu hiyo vizuri katika kujiletea maendeleo.
“Vikao ndani ya taasisi ni afya kwa taasisi na wafanyakazi kutokana na kutoa fursa kwa watumishi kuzungumzia masuala na changamoto wanazo kabiliana nazo” alisema.
Katibu Mkuu ametoa rai kwa wafanyakazi kutumia vikao halali kutoa mawazo yao badala ya kuzungumza katika maeneo yasiyo rasmi na kuwataka watumishi wapendane na kuheshimiana. Ameongeza kuwa siri ya mafanikio katika taasisi ni ushirikiano na kuwataka wafanyakazi wa NIDA kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kwa kushirikiana ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Kuhusu hatua iliyotangazwa na serikali ya kuiunganisha NIDA na RITA Gugu, amewataka watumishi kutokuwa na mawazo hasi na kinzani inapotokea mabadiliko kama hayo kwani Serikali ina dhamira njema na kwamba ajira za watumishi zitalindwa.
Amewataka watumishi wa NIDA kutekeleza majukumu kwa kuzingatia 4Rs za Mheshimwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa sababu ni sehemu ya maisha ya mtumishi mmoja mmoja na taasisi kwa ujumla.
Amewahakikishia wafanyakazi na menejimenti ya NIDA kwamba, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kutoa ushirikiano kwa NIDA ili kuhakikisha inaendelea kutoa huduma za Usajili na Utambuzi wa Watu kwa wananchi kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.
Kikao cha 26 cha Baraza la Wafanyakazi wa NIDA kilifanyika Novemba 22, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dar es Salaam.