NIDA Yasajili Wanachuo Wapya CBE

Na: Hadija Maloya – Dar es Salaam

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Ofisi ya Ilala kwa kushirikiana na Uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam wanaendesha zoezi la usajili wa wanachuo wa mwaka wa kwanza.

Zoezi hilo linafanyika katika viwanja vya chuo hicho kuanzia mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2024 ili kurahisisha upatikanaji wa Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) maarufu kama Namba za NIDA ambazo ni hitaji mojawapo la msingi kwa mwanachuo kuweza kujiunga na masomo ya elimu ya juu.

Akielezea zaidi Mratibu wa zoezi hilo kutoka CBE amesema kutokana na uzoefu wa miaka ya nyuma kumekuwa na tatizo kwa baadhi ya wananchuo wapya kutokuwa na Namba za NIDA ambazo hutumika katika udahili wa wanachuo wapya wanapojiunga chuoni hapo.

“Kwa kulifahamu hilo, Uongozi wa Chuo uliwasiliana na NIDA kuomba kupatiwa elimu na huduma ya usajili chuoni hapa ili kuondoa changamoto ya ukosekanaji wa Namba za NIDA kwa wanachuo wapya wanaojiunga na chuo hiki, hususan wale ambao  hawajawahi kujisajili huko walikotoka.” alisema Mratibu wa zoezi hilo.

Kwa upande wake Afisa Usajili Wilaya ya Ilala, Ndugu Mukobo Etimba amesema NIDA imefanikiwa kusajili zaidi ya nusu ya idadi ya jumla iliyotarajiwa wiki moja kabla ya kuhitimishwa kwa zoezi hilo “katika zoezi hili tunatarajia kusajili wanachuo wapya wapatao 505 lakini kufikia Oktoba 30, 2024 tumeweza kusajili wananchuo 303 ambao ni zaidi ya nusu ya matarajio” alisema Ndugu Etimba.

Katika kufanikisha zoezi hilo, Maafisa wa NIDA wakiongozwa na ndugu Njidan Ringo, Afisa Usajili Ofisi ya NIDA Ilala  walipata nafasi ya kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu Vitambulisho vya Taifa, hasa kuhusu mahitaji ya usajili, umuhimu wa Kitambulisho cha Taifa pamoja na namna ya kufanya mabadiliko ya taarifa zilizomo kwenye Kitambulisho cha Taifa.

 “Oktoba 21, 2024 tulipata nafasi ya kutoa elimu  kwa wanachuo wapya jinsi ya kujaza fomu ya maombi na kujisajili ili kupata namba na hatimaye Kitambulisho cha Taifa kwa kuanisha taratibu na mahitaji ya Usajili ikiwemo viambatisho vinavyohitajika, matumizi, umuhimu wa Kitambulisho na taratibu za kufuata endapo mtu anahitaji kubadilisha taarifa zilizopo kwenye kitambulisho chake” alisema.

Zoezi la usajili kwa wananchuo hao wapya limepangwa kufanyika kwa muda wa wiki mbili chuoni hapo kuanzia Oktoba, 22 hadi Novemba 04, 2024 baada ya hapo huduma ya usajili itapatikana katika Ofisi za NIDA wilayani pamoja na Vituo vya Huduma Pamoja vya Posta Mpya na Anartouglo-Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu