Na: Thomas Nyakabengwe – NIDA
Ukiuliza NIDA ni nini? watu wengi aghalabu wote kwa Tanzania watajibu kwamba ni Taasisi inayotoa Vitambulisho vya Taifa.
Ni kweli pasi na shaka kwamba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ndicho chombo chenye wajibu wa kutoa huduma za utambuzi zinazotambulika kitaifa na kimataifa na kutoa Vitambulisho kwa Watanzania na Wageni Wakaazi waishio kihalali nchini Tanzania.
Jukumu jingine ni Kuunda, Kusimamia na Kutunza Mfumo Mkuu wa Taifa wa Utambuzi wa Watu wa Kielektroniki wenye kuhifadhi taarifa sahihi za watu wote wanaoishi nchini na kushirikishana taarifa hizo na mifumo mingine ya Serikali na sekta binafsi kwa lengo la kuimarisha Usalama na Amani, Kiuchumi na Kijamii kwa Maendeleo ya Taifa.
Lakini jukumu hili la pili la NIDA ambalo ndilo jukumu kuu na
msingi wa kuanzishwa kwake (Utambuzi), halifahamiki miongoni mwa Watanzania
wengi isipokuwa kwa taasisi chache ambazo zimenufaika na huduma ya
kushirikishana taarifa ‘data sharing’ na kurahisisha utambuzi wa wateja wao
kielektroniki (eKYC).
Jukumu la Utambuzi wa Watu halitekelezwi na NIDA peke yake. Ni jukumu mtambuka linaloshirikisha wananchi, taasisi nyingine na vyombo vya ulinzi na usalama.
Ikumbukwe, utoaji wa Vitambulisho vya Taifa (Kadi) kwa raia, wageni wakaazi na wakimbizi ni matokeo ya shughuli ya Usajili na Utambuzi wa Watu ambayo imefanyika kwa ufasaha nchi nzima (Tanzania Bara na Zanzibar).
Ndio maana mwombaji anapokuwa amekamilisha usajili na kukidhi vigezo vya utambuzi kwanza anapatiwa Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) ambayo inamtambulisha anapotaka kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi hata kama hajapata Kitambulisho cha Taifa (Kadi).