NIDA Yazindua Namba Mpya ya Huduma kwa Mteja

Na: Musa Kadiko – NIDA

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeendelea kuboresha huduma kwa wananchi kwa kuboresha Kituo chake cha Huduma kwa Mteja ambapo imeweka mifumo mipya, vifaa vya kisasa na namba mpya ya huduma kwa mteja.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati, Geofrey Tengeneza wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika  makao makuu ya NIDA, Dar es Salaam.

Alisema maboresho yaliyofanyika katika Kituo cha Huduma kwa Mteja yatapanua wigo wa kuwahudumia wateja kwa kuwasiliana na mteja kwa urahisi na haraka hivyo kuongeza kasi katika kutoa huduma.

“Kutokana na maboresho hayo napenda kuwafahamisha rasmi wadau wetu wote na umma kwa ujumla, kwamba kuanzia tarehe 28/10/2024 namba ya simu ya Huduma kwa Wateja itakayotumiwa na wadau na wananchi wote itakuwa ni ya line ya TTCL ambayo ni: 023 – 221 0500. Namba hii tayari inapatikana na baadhi ya wadau wameshaanza kuitumia” alisema.

Sambamba na uboreshaji wa kituo hicho, alisema NIDA imekuwa ikibuni na kuboresha mifumo yake mbalimbali kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma bora zaidi kwa wananchi.

“Mifumo iliyobuniwa katika miaka ya hivi karibuni ni Mfumo wa kujisajili kwa njia ya mtandao, Mfumo wa kumuwezesha mwananchi kutambua kitambulisho chake kama kimetoka na mahali kilipo, Mfumo wa kufahamu Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) kama imetoka au laah, Mfumo wa kupata Namba ya malipo (Control Number)” alisema Tengeneza.

Alisema NIDA inaendelea kuimarisha miundombinu yake ya usajili na utambuzi wa watu ambapo baadhi ya miundombinu ni mifumo mbalimbali ya usajili na utambuzi, mashine za kuchapisha vitambulisho na Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Center).

Comment on “NIDA Yazindua Namba Mpya ya Huduma kwa Mteja”

  1. Habibu Hussein says:

    Ni kwa namna gani mtu anaweza kufahamu kama kitambulisho chake kimeshazalishwa na mahali kilipo ili aweze kukifuata?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu