NIDA Yaendelea Kutoa Huduma Bora kwa Wateja

Na: Agnes Gerald

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake katika Wiki ya Huduma kwa Mteja kwa kutatua changamoto zao na mahitaji yanayohusiana na Usajili na Utambuzi wa Watu katika ofisi zake za Usajili za Wilaya zipatazo 153 na katika wilaya zote ambako vituo vya Huduma Jumuishi (One Stop Shop Center) vimefunguliwa na Serikali.

Akielezea namna NIDA, inavyoadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Geofrey Tengeneza, amesema NIDA, inawashukuru wateja wote waliotoa muda wao na kujitokeza kusajiliwa hadi kuiwezesha NIDA, kusajili wateja zaidi ya milioni 25.

Pamoja na kuwashukuru wananchi, pia ameelekeza shukrani zake kwa taasisi wadau zaidi ya 107 waliounganisha mifumo yao na mfumo wa Utambuzi wa Watu kwani wamewezesha kitendawili cha mifumo kuzungumza kuteguliwa.

Alisema kwamba suala la Utambuzi, Ujenzi wa Mfumo Mkuu wa Utambuzi wa Watu na Ushirikishanaji Taarifa, lilikuwa ni ndoto ya miaka mingi ambayo sasa imekuwa kweli, kukamilika kwake kumewezesha wadau kutambua wateja wao kwa urahisi na usalama wa hali ya juu kutokana na mfumo huu kuwa na njia mbalimbali ambazo mdau anaweza kuzitumia kutambua wateja wake kimahsusi kabla ya kuwapatia huduma na kuwa na hakika ya Wateja  anaowahudumia”

Akielezea matokeo ya kuimarika kwa kutoa huduma bora kwa wateja, Tengeneza amesema wamekuwa wakitoa mrejesho kwa wateja wao kwa weledi kupitia namba mpya ya Kituo cha Huduma kwa Mteja waliyoitambulisha hivi karibuni 023 2210500, eMrejesho, baruapepe info@nida.go.tz, Tovuti www.nida.go.tz, Mitandao ya Kijamii X, Facebook na Instagram akiamini ndiko kulikopelekea NIDA, kutunukiwa Cheti kwa kuibuka Mshindi wa Kwanza katika kutoa Mrejesho kwa Wateja miongoni mwa Idara zilizoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Fedha na Utawala, Aida Tesha, amewaasa watumishi kuendelea kuwa wabunifu, kutoa huduma yenye tija kwa taasisi na kujenga uhusiano mzuri na wateja.

“Huduma bora ni kukutana na hitaji la Mteja kwa kumpatia utatuzi na ikibidi kutatua changamoto ya mteja zaidi ya matarajio yake hii ikimaanisha ‘above and beyond’ na ndio kauli mbiu ya wiki hii adhimu“ alisema.

Akisisitiza umuhimu wa wiki hii, amesema ni muhimu sana kwani inakumbusha watumishi sababu ya kuwa kazini na kusisitiza uwajibikaji na uadilifu kwa wateja.

Amehitimisha kwa kuwashukuru watumishi wote kwa juhudi walizozifanya katika kutoa huduma bora kulikoiwezesha NIDA, kutunukiwa Cheti cha Mshindi wa Kwanza katika kutoa Mrejesho kwa Wateja wake kwa mwaka 2023/2024.

Deusdedit Buberwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mamalaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), akipokea Cheti kutokana na NIDA kuwa Mshindi wa kwanza
katika kutoa Mrejesho kwa Wateja wake kwa mwaka 2023/2024 na Mhe. Waziri waMambo ya Ndani ya Nchi, Mha. Hamad Masauni.
Bi Atwabi Kwipunda akifurahi, punde baada ya kupatiwa Kitambulisho chake cha Taifa na Afisa Usajili katika moja ya ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),
Abdallah Mmanga Omar, Mkurugenzi Ofisi ya Uratibu Zanzibar, akitoa elimu kwa Wadau kuhusu Umuhimu Kuunganisha Mfumo wa kutoa huduma kwa wateja na wa Utambuzi wa Watu unaosimamiwa na NIDA, huku akitaja baadhi ya manufaa yake ikiwa ni kurahisisha Utambuzi wa wateja kutokanana Umadhubuti wa mfumo, kuweza kujibu Maswali Makuu Manne, NANI NI NANI? YUKO WAPI?, ANAFANYA NINI? NA ANAMILIKI NINI KATIKA TAIFA HILI?
Wateja Wakiendelea kupatiwa huduma za Usajili na Utambuzi wa Watu kwa nyakati tofauti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu