Kongamano la Ufuatiliaji na Tathmini

NIDA Yapongezwa kwa Kurahisisha Utambuzi wa Wateja Kimtandao

Na: Agnes Gerald – NIDA

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imepongezwa kwa kuziwezesha taasisi za Serikali na binafsi kutambua wateja wao kirahisi na kupatiwa huduma za kijamii na kiuchumi.

Pongezi hizo zimetolewa na wananchi na washiriki wa Maonesho ya Kongamano la Tatu la Ufuatiliaji na Tathmini waliotembelea Banda NIDA.

Mkaazi wa Uwanja wa Ndege, Shabani Ali alikiri NIDA kupiga hatua kiutendaji kwa sababu yeye na wazazi wake wana Utambulisho wa Taifa uliomwezesha kupata mkopo wa Elimu ya Juu na baadaye ajira ambayo hivi sasa imemwezesha kujikimu kimaisha na kuwasaidia wazazi na ndugu zake.

Wadau pia hawakua nyuma katika kutoa tathmini yao kuhusu matokeo chanya na faida lukuki walizozipata baada ya kuunganisha mifumo yao ya utoaji huduma na Mfumo Mkuu wa Taifa wa Usajili na Utambuzi wa Watu kwa sababu umewasaidia kutoa huduma kwa wateja wao kirahisi na salama zaidi.

Mtaalamu wa TEHAMA kutoka TASAF, Peter Lwanda anasema wamenufaika na matumizi ya mfumo kwani unawasaidia katika kuhakiki taarifa za walengwa wa misaada ya kaya masikini kwa kuweza kuoanisha tarifa za umri, makazi, uraia hasa kwa wanaoishi katika mikoa iliyopakana na nchi jirani.

Naye Meneja Uhusiano na Biashara wa CRDB, Flora Urio anasema tangu mfumo wao ulipoanza kuzungumza na NIDA, imewarahisishia kufanya maamuzi sahihi na salama wakati wa kutoa huduma kwa wateja wao, kuanzia hatua ya kufungua akaunti, utoaji fedha na kutoa mikopo kwani sasa wanahakika ya mteja wanayemhudumia kuwa ndiye kutokana na Mfumo wa NIDA kuweza kujibu maswali makuu manne, Nani Ni Nani? Yuko Wapi? Anafanya Nini Na Anamiliki Nini?

Meneja wa PSSF Zanzibar, Jafari Mgala anasema kwa sasa wananchi wanapatiwa mafao yao ndani ya muda mchache akikiri kuwa pamoja na maboresho mbalimbali ya kihuduma na kimifumo ambayo PSSF imekuwa ikiyafanya, NIDA ina mchango mkubwa kwani kwa PSSF kujiunga na Kanzidata ya NIDA kumechochea spidi ya utoaji huduma kuongezeka kwa kuweza kuwatambua wateja wao kwa kutumia Namba ya Utambulisho wa Taifa ambayo ni alama inayomtambulisha msaafu na wateja wengine kimahsusi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uelimishaji Umma kutoka TAKUKURU, Matai Kirumbi anasema uwepo wa mfumo huu ni chachu ya ongezeko la uwazi, uwajibikaji na kuimarishwa kwa usalama kwa raia na mali zao.

Katika maonesho hayo, NIDA imefanikiwa kutoa elimu na huduma ya Usajili na Utambuzi wa Watu kwa wananchi zaidi ya 300 ambapo pamoja na huduma nyingine zilizotolewa katika banda la NIDA, wateja wengi waliokuwa wameshakamilisha Usajili walipatiwa NIN.

Maonesho na Kongamano vilifunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullakwa Niaba ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Hotel ya Golden Tulip, uliopo Uwanja wa Ndege Zanzibar Setemba 17, 2024 na kufungwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Doto Biteko Septemba 20, 2024. Maonesho ya Kongamano la Ufuatiliaji na Tathmini yalihudhuriwa na tasisi 22 na watu zaidi ya 650 walishiriki Kongamano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Taarifa Kwa Umma

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu