NIDA Yaongeza Hamasa Maonesho ya Biashara Tanga

Na. Calvin Minja

Katika kuunga juhudu za kukuza uchumi, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeendelea kushiriki maonyesho ya 11 ya Biashara Tanga yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara.

Maonyesho hayo yanaratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).

Maonyesho hayo yalianza Mei 28, 2024 na kuzinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian,  Juni 03, 2024 yanategemea kufikia kilele chake tarehe  6 Juni, 2024.

Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mkoa wa Tanga, Hawa Hamadi, pamoja na Afisa Tehama, Habib Mshana, wakitoa elimu kwa wananchi na wadau waliotembelea banda la NIDA, kwenye Maonesho ya 11 ya Biashara na Utalii ya Tanga, yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, kuanzia tarehe 28 Mei hadi 06 Juni, 2024.

Dkt. Burian amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kuona fursa mbalimbali zinazotolewa na wafanya biashara wa mkoa wa Tanga lakini pia amewataka watu kutoka maeneo tofauti kuja kujionea fursa tofauti zinazopatikana kwenye Jiji la Tanga.

Kwenye maonyesho hayo ya 11 ya Biashara na Utalii, NIDA imewasogezea wananchi huduma mbalimbali ikiwemo kufahamu mahali Kitambulisho kilipo, kufahamu Namba ya Utambulisho wa Taifa, namna ya kujaza fomu ya usajili kwa usahihi, Namna ya kujisajili kwa njia ya mtandao, utaratibu unaopaswa kufuata wakati wa mabadiliko  ya taarifa na mahitaji muhumu yanayohitajika wakati wa usajili.

Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mkoa wa Tanga, Hawa Hamadi, na Namghanga Msuya, Afisa Usajili Msaidizi Mwandamizi wa Ofisi ya Usajili ya NIDA, mkoani Tanga, wakitoa huduma za Usajili na Utambuzi wa Watu ikiwemo kufahamu iwapo Vitambulisho vya Taifa vimetoka, kwa Wageni Wakaazi waliojitokeza kwenye Maonesho ya 11 ya Biashara Tanga, yaliofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, kuanzia tarehe 28 Mei hadi 06 Juni, 2024

Akizungumza wakati wa maonesho hayo kwenye banda la NIDA, Afisa Msajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mkoa wa Tanga, Hawa Hamadi, amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kwani wamejipanga kuwahudumia wananchi wote ambao watajitokeza kwenye banda la NIDA.

“Wananchi wote mnakaribishwa kwenye banda letu, tumejiandaa vilivyo, kuwahudumia na tumekuja hapa kwa ajili yenu.” alisema Hawa.

Afisa Habari wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Ndg. Calvin Minja akitoa Elimu kwa mjasiriamali, mkaazi wa Tanga, kuhusu namna ya kujaza fomu ya maombi ya Utambulisho wa Taifa kwa usahihi wakati alipotembelea banda la NIDA kwenye Maonyesho ya 11 ya Biashara Tanga, yaliofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, kuanzia tarehe 28 Mei hadi 06 Juni, 2024.

Kwa upande wa Afisa Habari Mwandamizi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Agnes Gerald  amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwenye banda la NIDA kwa ajili ya kupata elimu juu ya huduma mbalimbali ambazo NIDA inazitoa.

“Tumekua tukishiriki maonyesho haya ya Biashara Tanga, muitikio wa watu ni mkubwa ambao wanafika kwenye banda letu, tunatoa wito kwa wote ambao wanachangamoto zozote juu ya huduma zetu kufika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

“Tunaendelea kusisitiza wananchi kuendelea kujitokeza kujisajili kwa wakati na kuepuka kusubiri matukio kama ajira au dharula ili iwe rahisi kwao kufanikisha azma walizokusudia.

“Lakini pia nitoe wito kwa wakazi wa Tanga na vitongoji vyake kujitokeza kwenye Ofisi za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuchukua vitambulisho vyao ili waweze kuvitumia vitambulisho hivyo katika kupata huduma za kijamii na kiuchumi kirahisi.” alisema Agnes.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu