Na: Thomas Nyakabengwe – NIDA
Wakazi wa Mkoa wa Kagera wamejitokeza kwa wingi katika zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Waombaji wa Vitambulisho vya Taifa zilizokuwa na mapungufu mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Ofisa Usajili Wilaya ya Kyerwa, Anna Kapwela alisema wananchi wengi wameitikia wito wa kuja kuhakiki na kurekebisha taarifa zao ili wapate Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN).
Alisema mwitiko huo umetokana na uhamasishaji mkubwa na matangazo yaliyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na wadau mbalimbali ambapo matangazo yametolewa kwenye redio, magari ya matangazo (PA), ujumbe wa simu za mkononi (Bulk SMS), nyumba za ibada na viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji.
Alisema wengi wamefanikiwa kurekebisha upungufu uliokuwapo kwenye maombi yao na kukidhi vigezo vya kupata NIN.
Hata hivyo, alisema baadhi ya waombaji hawajafanikiwa kutatua upungufu uliokuwapo kwenye maombi yao na kuelekezwa kuwasilisha vielelezo vinavyotakiwa ili kukamilisha maombi yao.
Alitoa wito kwa waombaji ambao hawajahakiki taarifa zao kujitokeza kuhakiki kwa kuwa huduma hiyo imesogezwa kwenye kata wanazoishi ili kukamilisha maombi yao bila kulazimika kwenda kenye ofisi za NIDA.
Zoezi hilo lililoanza Mei 29, 2023 linafanyika katika wilaya zote za Kagera na linatarajiwa kukamilika Juni 16, 2023.