MASHINDANO YA MEI MOSI 2023 YAHITIMISHWA MKOANI MOROGORO

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Mashindano ya Kombe la Mei Mosi 2023 yamehitimishwa mkoani Morogoro kwa timu zilizofanya vizuri katika michuano hiyo kukabidhiwa makombe, medali na vyeti kwa timu zote zilizoshiriki mashindano hayo yakiwa ni shamrashara za kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani.

Akifunga mashindano hayo mkoani Morogoro Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Kaspar Mmuya amesema mashindano hayo yamewasaidia watumishi kujenga afya ya mwili na akili na kuongeza ari ya kufanya kazi na kutoa huduma stahiki kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi.

Bw. Mmuya amewataka waajiri kuendelea kuwapa fursa wafanyakazi kushiriki michezo ya Mei Mosi kila mwaka ikiwemo Wizara, taasisi, mikoa, wakala wa serikali, halmashauri, Ofisi za Wakuu wa Mikoa pamoja na sekta binafsi kutenga muda na kuwapa watumishi fursa ya kushiriki mashindano hayo kila mwaka yanapofanyika maadhimisho hayo kitaifa.

Akimkaribisha mgeni Rasmi katika hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Masamu amesema michezo ya mwaka huu imeshirikisha wanamichezo kutoka katika Wizara, mashirika na taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi kutoka klabu 39 wakiwa jumla ya wachezaji 2330 ambao wameshiriki michezo mbalimbali.

Bi. Masamu ameongeza kuwa Kamati ya Mei Mosi Taifa inahamasisha Wizara, Idara na taasisi ambazo hazikushiriki mashindano hayo watenge bajeti ambayo itawezesha timu zao kushiriki mashindano hayo ikizingatiwa michezo huleta hamasa katika utendaji kazi.

Katika kuhitimisha mashindano hayo timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefanya vizuri katika michezo yake na kuibuka mshindi wa kwanza wa jumla huku ushindi wa pili umekwenda kwa timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi).

Aidha, katika hafla hiyo zimeshuhudiwa fainali za mchezo wa mpira wa miguu, netiboli pamoja na mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume na wanawake. Kwa upande wa mpira wa miguu bingwa ni timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, mshindi wa pili ni timu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na mshindi wa tatu ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kwa upande wa mchezo wa netiboli bingwa ni Ofisi ya Rais Ikulu wakifuatiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi huku nafasi ya tatu ikienda kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Katika mchezo wa kamba wanaume bingwa ni timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi), mshindi wa pili ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na mshindi wa tatu ni Ofisi ya Rais Ikulu wakati kwa upande wa wanawake bingwa ni timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi), mshindi wa pili ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na mshindi wa tatu ni Wizara ya Afya.

Washindi wa makombe mengi na Mshindi wa jumla Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakiwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Kaspar Mmuya pamoja na Mkurugenzi wa Rasilimali watu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakiwa na wanamichezo wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakishangilia ushindi wa Jumla wa Mashindano ya Mei Mosi Taifa yaliyofanyika Mkoani Morogoro yaliyofikia kilele tarehe 29 Aprili 2023.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu