NIDA Ilala Yaadhimisha Muungano kwa Kuyafikia Masoko 17

Na: Agnes Gerald – NIDA

Ofisi ya Usajili ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wilaya ya Ilala imeadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kutoa huduma ya Usajili na Utambuzi wa Watu kwenye Masoko 17 yaliyoko katika wilaya hiyo.


Bw. John Etimba Afisa Usajili Wilaya ya Ilala, amesema kuwa wamesajili  wafanyabiashara katika masoko 17 ya Jiji la Ilala ambayo ni pamoja na Ilala, Mchikichini, Buguruni, Kisutu, Kigogo Freshi, Zingiziwa, Kilwa, Kigogo Sambusa, Tabata Muslim, Bombom, Vingunguti, Tabata Kimanga, Tabata Kinyerezi, Kigilagila, Minazi Mrefu, Feri na Machinga.

Alisema jitihada za kuenzi miaka 59 ya Muungano hazikuishia hapo bali wilaya ya Ilala imeyafikia makundi mbalimbali katika jamii na kuwapatia huduma ya Usajili na Utambuzi wa Watu pia wakiwemo wazee, wanafunzi, wenye mahitaji maalumu na wafanyabiashara wadogowadogo masokoni, wahitimu wanaofuatilia Utambulisho ili waombe ajira pamoja na makundi mengine mengi.

“Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kila jitihada ili kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kasi hivyo lazima na sisi katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku tunahakikisha tunaenda sanjari na kasi hiyo ili kuweka mazingira yanayowawezesha makundi hayo Kusajiliwa, Kutambuliwa na Kutambulishwa kwenye taasisi nyingine ili waweze kupatiwa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi bila kukwama,” alisema.

Ametoa rai kwa wananchi wote wanaofika kwenye Ofisi ya Usajili wilaya ya Ilala kupatiwa huduma kuhakikisha wanajaza taarifa zao kwa usahihi na kuweka viambatisho ambavyo majina yake yanaoana ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Habari Picha: Maafisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA), wilaya ya Ilala, wakitoa Huduma ya Usajili na Utambuzi wa Watu kwa makundi mbalimbali ya wananchi wa wilaya hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu