Serikali Yafuta Ukomo wa Matumizi ya Kitambulisho cha Taifa

Na: Mwandishi wetu – NIDA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Vitambulisho vya Taifa havitakuwa na muda ukomo wa matumizi.

Mhe. Waziri ametoa tamko hilo Februari 21, 2023 kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Idara ya Wakimbizi, Dar es Salaam.

Alisema yamefanyika marekebisho ya Kanuni za mwaka 2014 za Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu ya Mwaka 1986 kwa lengo la kutekeleza azma ya Serikali katika kuweka mazingira wezeshi kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuendelea kutekeleza majukumu yake ya Usajili, Utambuzi na Utoaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa raia, wageni wakaazi na wakimbizi kwa kasi.

Amezitaka taasisi mbalimbali kuendelea kutoa huduma kwa wananchi ambao vitambulisho vyao vimefikia tarehe ukomo ya matumizi bila kuwa bughudhi kwani vyote vinavyozalishwa sasa na vya zamani vitaendelea kutumika.

Kuhusu na matumizi ya Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN), Mhe. Masauni amewataka watoa huduma kwa umma hususan taasisi za Serikali kutowabugudhi wananchi kwa kuwadai Vitambulisho vya Taifa angali wana NIN kwani inamtambulisha mwanchi kipekee na kumtofautisha na mwananchi mwingine na NIN hiyo huwekwa juu ya Kitambulisho cha Taifa cha mwananchi husika.

Mhe. Masauni katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, pia alieleza kuhusu marekebisho ya Kanuni ya 16 na Jedwali la Pili la Kanuni hizo ambapo pamoja na mambo mengine inampa uwezo Waziri mwenye dhamana kufanya marekebisho ya ada zilizopo kwa kushirikiana na Waziri mwenye dhamana na Fedha na kuongeza pia Kanuni ya 17A itakayoweka sharti na takwa la kisheria kwa taasisi inayokusudia kutumia taarifa za Kanzidata ya NIDA kuzingatia taratibu zitakazowekwa ikiwa ni pamoja na kutuma maombi kwa kutumia fomu maalum ya maombi na kuingia Mkataba wa Ushirikishanaji Taarifa (DataSharing Contract) na NIDA kuwa na uwezo wa kusimamisha huduma hiyo iwapo taratibu zitakiukwa.

“Mchakato wa Marekebisho ya Kanuni umekamilika na tayari Kanuni hizo zimeanza kutumika baada ya kutangazwa rasmi kwa Tangazo la Serikali (GN) Na. 96 la tarehe 17 Februari, 2023. Hivyo, Serikali inatoa rai kwa watoa huduma wote nchini wanaotumia Utambulisho wa Taifa kutoa huduma kwa wananchi hususan, taasisi za fedha, benki na kampuni za simu kuendelea kuvitambua na kuvitumia Vitambulisho vya Taifa ambavyo vina tarehe ya muda wa ukomo uliopita kwa kuwa Vitambulisho hivyo havitakuwa na ukomo wa matumizi. Aidha, marekebisho haya hayahusishi Vitambulisho vya Wageni Wakaazi na Wakimbizi na hivyo muda wa Vitambulisho hivyo uzingatiwe”.

Alihitimisha kwa kutoa maelekezo kwa Maafisa Usajili wote wa NIDA kuendelea kutoa ufafanuzi na ushirikiano kwa wananchi pindi wanapofika katika Ofisi za Usajili za NIDA kupata maelezo au ufafanuzi kuhusiana na matumizi ya Vitambulisho vilivyo na tarehe ya ukomo iliyokwishapita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu