Wanawake waaswa kuacha kukumbatia tamaduni zisizofaa

Na Hadija Maloya.

Wanawake mkoani Dar es salaam wameaswa kutokukumbatia na kufuata tamaduni zinazolenga kuwakandamiza na kuwanyima haki zao mbalimbali na hivyo kuwafanya waendeleee kujiona wanyonge na kurudisha nyuma maendeleo yao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda alipokuwa akihutubia Wanawake kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika tarehe 08 ya mwezi Machi kila mwaka, ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, maadhimisho hayo yamefanyika kwenye Viwanja vya Leaders Club vilivyopo katika Manispaa ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Akiainisha tamaduni hizo, Bwana Paul Makonda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo mkoani Dar es salaam alisema kuwa ni pamoja na baadhi ya makabila kuona Wanawake hawapaswi kushirikishwa katika mambo ya msingi kama vile kutoa maamuzi, kurithi mali kwenye familia pindi waume zao wanapofariki, kutoruhusiwa kuhoji kitu mbele ya Baba, kutoruhusiwa kuanzisha au kufanya shughuli yoyote ya kimaendeleo, au Wanawake wengine kusubiri hadi aamuliwe na mtu mwingine hasa mwanaume (baba) hata kama mumewe anampa kibali cha kufanya shughuli za uzalishaji.

Kutokana na mila na tamaduni hizo zisizofaa, Mhe. Makonda amewataka Wanawake na jamii yote kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya tamaduni kandamizi. “Ni lazima Wanawake na jamii kwa ujumla tushikamane katika kuhakikisha tunatokomeza mila zote zinazokandamiza haki zenu katika ngazi zote kuanzia kwenye familia zenu’ alisema.

Kuhusu baadhi ya sheria zinazoonekana kuwa kandamizi kwa ustawi na maendeleo ya Wanawake,  Mhe. Makonda amebainisha kuwa amezungumza na Waziri wa Afya, Jinsia Wanawake, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, ili kuangalia uwezekano wa kufanyia marekebisho sheria ikiwemo sheria ya Ndoa na Mirathi kwani imepitwa na wakati. “Sheria hii ikifanyiwa marekebisho itawalinda Wanawake na watoto hasa katika masuala ya mirathi” alisema.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es salaam amewataka Wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani wana uwezo mkubwa wa uongozi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya kisiasa. Ametolea mfano kuwa Wanawake ni walezi na wasimamizi wazuri wa uchumi katika familia ikilinganishwa na wanaume.

Mkuu huyo wa mkoa amewatahadharisha Wanawake wenye tabia ya kuwatolea watoto maneno makali na mabaya kutokana na hasira pale inapotokea sintofahamu baina yake na mwenzi wake na kuwataka kuacha kufanya hivyo kwani wanasababisha utovu wa nidhamu kwa watoto wao na hatimaye kuathiri familia, jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla.

Aidha amewataka pia wanaume wenye tabia ya kupiga wake zao kuacha tabia hiyo mara moja na kuahidi kuwa yeyote atakayekaidi, basi atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Katika kuonyesha msisitizo juu ya agizo lake hilo  Mhe. Makonda ametoa namba ya simu kwa Wanawake ili kuripoti kwake wanapopigwa na waume zao.

Maadhimisho ya siku ya Wanawake yameadhimishwa nchini Kitaifa mkoani Simiyu ambapo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.

Watumishi Wanawake wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es salaam tarehe 08 Machi, 2020.
Katibu wa Kamati ya Wanawake ya Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) tawi a NIDA Bi. Sechelela Malecela (aliyesimama mbele) akihamasisha jambo kwa Watumishi Wanawake wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) muda mfupi kabla ya maandamano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu