Na Agnes Gerald, NIDA
Watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na kutunza siri.
Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima alipofungua Baraza la Wafanyakazi Februari 24, 2020 katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Polisi, Dar es Salaam.
Amewataka watumishi wa NIDA kuzingatia maadili katika utekelezaji wa shughuli za Usajili za Mamlaka pindi wanapotoa huduma kwa wananchi. Amewataka Watumishi wa NIDA kufanya kazi kwa bidii ili wananchi wapatiwe huduma kwa wakati pamoja na kutunza siri za taasisi kwani kufanikiwa ama kutofanikiwa kwa NIDA kuko mkononi mwa kila mtumishi hivyo kila mtumishi asimame kwenye nafasi yake kwa kutimiza wajibu wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Dkt. Arnold Kihaule aliwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mamlaka hadi kufikia Desemba 2019 ambapo ameeleza idadi kubwa ya wananchi wameshasajiliwa na kupatiwa Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) ambazo zinatumika kusajili laini za simu, kufungua akaunti za benki, kukata leseni ya udereva, biashara, Kupata Namba ya Mlipa Kodi (TIN), kuomba ajira serikalini na huduma nyinginezo.
Aidha katika taarifa yake ameelezea baadhi ya changamoto zinazowakabili moja wapo ni kwa wananchi kutokuwa na viambata vya kutosha vya kuthibitisha uraia, umri na makazi na kueleza ambavyo NIDA imejitahidi kutoa elimu kwa umma katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Akizungumzia utaratibu wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Wafanyakazi Serikali Kuu na Afya (TUGHE), Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Tabu Mambo amewataka wajumbe kuhakikisha wanachagua Katibu wa Baraza kwa kufuata utaratibu, kumpima mgombea kama anatosha na kila mjumbe kuhakikisha anatumia haki yake ya msingi kupiga kura.
Vikao vya Baraza la Wafanyakazi serikalini vipo kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2002, Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma Na.19 ya mwaka 2003, pamoja na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004.