Wananchi kupata Vitambulisho vyao ndani ya muda mfupi

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)ni miongoni mwa Taasisi za Serikali zinazoshiriki maonyesho ya Kitaifa ya Nanenane, yanayofanyika katika Mkoa wa Lindi katika viwanja vya  Ngongo.

Maonyesho hayo ambayo yamezinduliwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene; ambaye amewaasili na kukagua baadhi ya mabanda kabla kuwahutubia wananchi wa Lindi waliokusanyika kwa wingi kushuhudia tukio hilo.

NIDA inashiriki kwenye maonyesho hayo kwa kutoa huduma ya Usajili kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi ambapo kwa wale watakaokamilisha taratibu zote za Usajili watapatiwa Vitambulisho vyao ndani ya mwezi mmoja. Huduma nyingine zinazotolewa ni pamoja na Ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi ambao walisajiliwa kwenye maonyesho hayo mwaka Jana, wananchi kupata taarifa za vitambulisho vyao kwa wale ambao wamekamilisha taratibu za Usajili, elimu kuhusu matumizi, faida na umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa pamoja na kusoma taarifa za mwananchi kwenye Kitambulisho chake kutumia Tovuti Salama iliyoundwa kurahisisha matumizi ya  vitambulisho vya Taifa.

Kauli Mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu “Zalisha kwa Tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi ili kufikia uchumi wa kati”. Ili kufikia malengo haya; kupitia mfumo wa Taifa wa Usajili na Utambuzi wa Watu kuwatambua Wakulima na Wafugaji, uzalishaji wenye tija na ufugaji wa kisasa unawezekana. Hivyo wananchi wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kusajiliwa ili kunufaika na manufaa mapana ya mfumo huu katika kuinua uchumi na maendeleo ya Taifa.

Maonyesho ya Nanenane Kitaifa yanafanyika kwa awamu ya Nne mkoani Lindi ili kutoa fursa pana kwa wakulima na wafugaji kunufaika na elimu pana inayotolewa na Taasisi na Mashirika mbalimbali kwa lengo la kufanikisha ndoto kubwa ya Taifa la Uchumi wa Kati.

 

Mmoja wa wananchi wa Lindi akipata maelekezo toka kwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NIDA, Bi. Rose Mdami.

 

Baadhi ya Wananchi waliotembelea Banda la NIDA wakifuatilia maelelezo ya namna ya kujisajili toka kwa Afisa Usajili mkoa wa Lindi Ndugu Oliver Walles Mahinya.

 

Wananchi wa Mkoa wa Lindi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi rasmi wa maonyesho ya Kitaifa ya Nananenane yanayofanyika mkoani humo kwenye viwanja vya Ngongo. Maonyesho ya Nanenane yaliasisiwa mwaka 1990 mkoani Mbeya na yameendelea kwa mzunguko kwa kila mkoa kupata fursa ya kuandaa na kushiriki.

 

Kikundi cha jadi kikitumbuiza wakati wa uzinduzi wa Maonyesho ya Nanenane Viwanja vya Ngongo Lindi.

 

Banda la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa katika viwanja ya Ngongo, karibu kabisa na Jukwaa Kuu la Maonyesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Taarifa Kwa Umma

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu