Watanzania kuanza kunufaika na matumizi ya utambulisho wa Taifa(NIN)

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; Mh. Mwigulu Nchemba (Mb) leo ametembelea Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambapo alikutana na Menejimenti ya NIDA na kupokea taarifa ya maendeleo ya shughuli ya Usajili na Utambuzi wa Watu.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa Vitambulisho vya Taifa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA; Ndugu Andrew Wilson Massawe, amemweleza Mh. Waziri mpaka sasa NIDA imekamilisha awamu ya kwanza ya usajili wa Watumishi wa Umma, ambapo watumishi 500,605 wamesajiliwa nchi nzima. Kwa sasa NIDA inaendelea na hatua ya mwisho kukamilisha uhakiki wa watumishi hao ili kutoa namba za utambulisho na kuunganisha Kanzi Data ya NIDA na Utumishi, ambapo watumishi watakuwa wakitambuliwa kwa alama zao za vidole.

Mbali na kukamilisha Usajili wa Watumishi; NIDA imepanga kuanza kutoa namba za Utambulisho wa Taifa kwa wananchi wote nchi nzima waliosajili kwenye daftrati la NEC. Namba hizo zitawawezesha kuanza kunufaika na utambulisho wa Taifa kwa kupata baadhi ya huduma toka kwa wadau mbalimbali wakati wakiendelea na taratibu za kukamilisha usajili wao ili kupata vitambulisho vya Taifa.

Kwasasa NIDA ina taasisi na mashirika 35 ambayo yameanza kutumia Kanzi Data (Database) kuhakiki wateja wanaofika kupata huduma zikiwemo taasisi za fedha; huku Taasisi na kampuni nyingine 70 zimeonyesha nia ya kutumia mfumo huo kuhakiki taarifa za wateja wanaowapa huduma.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Mwigulu amesema hii ni fursa ya pekee kwa wananchi kuhakikisha wanapata nambari za utambulisho wa Taifa itakayowawezesha kuanza kunufaika na fursa mbalimbali zinazokosekana kwa sasa kutokana na Taifa kutokuwa na Vitambulisho vya Taifa. Amesema hatua hii nzuri na kubwa kwa Taifa, kwani katika muda mfupi asilimia kubwa ya watanzania watakuwa wameingizwa kwenye Kanzi Data (Database) ya NIDA na hivyo Serikali kuanza kutimiza ile ndoto ya miaka mingi ya Taifa kuwa na Kitambulisho cha Taifa.

“ Nia ya Serikali ni kuona kila mtu anatambulika na kupitia mfumo huu wa Utambuzi na Usajili kuwapunguzia watanzania mzigo wa kubeba kadi lukuki za utambulisho. Kwa kuwa mfumo huu ni wa kielektroniki una uwezo wa kufanya mambo mengi, hata kutumika kufanya malipo katika maduka makubwa na huduma nyingine muhimu na hivyo kurahisisha maisha ya kila mtanzania” alisisitiza

NIDA imepanga kuanza kutoa namba za utambulisho (National Identification Number – NIN) kwa wananchi wote waliosajiliwa katika daftari la Mpiga kura, zoezi ambalo limepangwa kuanza mwezi Desemba mwaka huu. Mbinu mbalimbali zitatumika kuhakikisha kila mtanzania aliyesajiliwa NEC  anapata namba yake pale alipo; pamoja na kutoa utaratibu wa namna ya kukamilisha usajili wake ili kupata utambulisho kamili. Zoezi hili halitahusisha wananchi ambao tayari wana Vitambulisho vya Taifa.

Aidha; Waziri Mwigulu amewaasa watanzania kuwa wazalendo linapofika suala la kuweka pingamizi kwa wale watu ambao siyo raia kwani lazima kabla ya kutoa kitambulisho lazima kila mwombaji kuhakikiwa na kuthibitishwa uraia wake kabla ya kupewa kitambulisho.

Hii ni ziara ya kwanza kwa Waziri Mwigulu kutembelea NIDA tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; ambapo mbali na kutembelea makao makuu ya NIDA na kufanya mazungumzo na Menejimenti pia alipata fursa ya kutembelea kituo cha uhifadhi na uchakataji Taarifa (Data Centre) na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na NIDA.

 

4681

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh. Mwigulu Nchemba (Mb) akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mkutano wa mamlaka ya vitamulisho vya Tafa (NIDA). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA, Ndugu Andrew Wilson Massawe na Bi. Angelina Shirima, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.

 

4697

Bi Oliver G Nyeriga Mwandishi wa habari kutoka East Africa Radio akimuuliza Swali Mh Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati akizungumza na waandishi wa Habari.

 

4699

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Ndugu Andrew Wilson Massawe, akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi  (aliyeketi kulia). Kushoto ni Bi. Angelina Shirima Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.

 

4709

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba kwenye picha ya pamoja na Menejementi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA.

 

4717

Kaimu mkurugenzi wa Idara ya Mifumo ya Komputa (Tehama) ndugu Mohamed Khamis Akifafanua namna mfumo wa AFIS inavyofanya kazi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alipotembelea kituo cha  kuhifadhi na kuchakata Taarifa Data Centre

 

4732

Afisa Usajili Bi. Jemimah Mulokozi akitoa maelezo ya namna kitengo cha uhakiki na udhibiti ubora NIDA kinavyofanya ukaguzi wa ubora wa kitambulisho mara baada ya kuzalishwa kabla ya kuanza kusambazwa katika vituo vya Usajili vya Wilaya kwa kugawanywa kwa wananchi.

 

4748

Mchambuzi wa mifumo ya kompyuta Bw. Sadiki Kiwia akifafanua namna mfumo wa mawasiliano ya Tehama unavyosimamiwa kutoka kwenye vituo vyote vya Wilaya nchi nzima.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Taarifa Kwa Umma

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu