Nida kushiriki maonesho ya 23 ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Lindi kuanzia tarehe 01/08/2016 hadi tarehe 10/08/2016

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kushiriki Maadhimisho ya Maonyesho ya 23 ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Lindi kuanzia tarehe 01/08/2016 hadi tarehe 10/08/2016 ili kutumia fursa ya maonyesho hayo kutoa elimu kwa umma juu ya mchango mkubwa NIDA ilionao katika maendeleo ya sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Kauli mbiu ya maonyesho hayo “Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Nguzo ya Maendeleo, Vijana Shiriki Kikamilifu hapa Kazi Tu”. Kwa kauli mbiu hiyo NIDA imeona ni vyema ikauhabarisha na kuuelimisha umma juu ya mchango mkubwa ilionao kwa maendeleo ya Wakulima, Wavuvi na Wafugaji. NIDA ni Chachu, Ufunguo na Nguzo ya maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Kitaifa na Kimataifa pia. Hii ni kutokana na moja ya jukumu lake ikiwa ni Ujenzi wa mfumo madhubuti na imara wenye kubeba taarifa sahihi za wakazi wote waishio nchini ikijumuisha raia (wananchi), wageni na wakimbizi waishio nchini kihalali ambao matokeo yake ni kutoa Kitambulisho cha Taifa chenye kutambulika Kitaifa na Kimataifa, kwani kwa taarifa hizo muhimu wananchi (Wakulima, Wavuvi na Wafugaji) wataweza kupata huduma za kijamii kirahisi.

Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa watu ambao matokeo yake ni kutoa Kitambulisho cha Taifa chini ya usimamizi wa NIDA, pia unamanufaa makubwa katika kuchochea ukuaji wa sekta ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo kwa kuwawezesha Wakulima, Wavuvi na Wafugaji kutambulika kirahisi, yeye ni nani, yuko wapi, anafanya nini na anamiliki nini katika Taifa hili, maswali ambayo ndiyo dhana kuu ya Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu unaosimamiwa na NIDA.

Kutambulika kirahisi kwa Wakulima, Wavuvi na Wafugaji kunawapatia manufaa yafuatayo:

1. Mkulima, Mvuvi na Mfugaji kukopesheka kirahisi katika taasisi za kifedha kwa kuwa na nambari maalumu ya Utambulisho ama Kitambulisho cha Taifa.

2. Serikali kuweza kutoa ruzuku za pembejeo za kilimo na mbegu bora kwa wakulima kirahisi kwani kupitia mfumo wa Utambuzi wa NIDA unaolenga kutoa Kitambulisho cha Taifa, ruzuku hizo kwenda kwa walengwa nufaika na kutimiza azma ya serikali ya Kilimo kwanza.

3. Serikali kuweza kutoa Zana za Uvuvi kwa walengwa nufaika kwani sasa kundi hilo kutambulika kirahisi kupitia mfumo wa NIDA unaolenga kutoa Kitambulisho cha Taifa.

4. Kwa wafugaji vilevile kutambulika kimahsusi, kulingana na shughuli wanayofanya, hivyo kuwa rahisi kupata huduma zitolewazo na serikali.

5. Kurahisisha zoezi la utoaji fidia za majanga kwa wahusika na majanga katika shughuli za kilimo, uvuvi na mifugo kama vile ya moto, mafuriko n.k iwapo yametokea, kwani taarifa zao muhimu kupatikana kwenye mfumo wa NIDA kwa waliosajiliwa.

6. Wakulima, Wavuvi na Wafugaji kunufaika na uwezeshaji na uwekezaji unaofanywa na sekta mbalimbali za uchumi zinazolenga kuinua uchumi wa makundi husika kwa kutoa mtaji wa kuwekeza katika Kilimo, Uvuvi na Ufugaji.

Ukiachilia mbali faida hizo, katika maonyesho hayo NIDA inatarajia kutoa huduma mbalimbali ambazo ni:

i. Kusajili na Kuchukua Alama za Kibaiolojia wananchi wote wa mkoa wa Lindi ambao hawajawahi kujisajili (Full Enrollment).

ii. Dawati la Huduma kwa Mteja kutolewa, ambapo Maafisa kutoka NIDA watakuwepo siku zote 10 za maonyesho kujibu maswali yote ambayo yamekuwa yanawatatiza wanachi na kuelimisha Umma kwa kina kuhusu Mfumo wa Usajili na Utambuzi wa Watu ambao matokeo yake ni kutoa Vitambulisho vya Taifa, faida zake pamoja na kuelezea hasara za kutokuwa na Utambulisho/Kitambulisho hicho.

iii. Dawati la kuelezea Sheria ya Mamlaka (Ijue Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu) kutolewa.

iv. Dawati la Tovuti Salama (Secure Portal) ya NIDA kuelezewa.

Banda la NIDA katika Maonyesho ya Nanenane ya 23 lipo eneo yalipo Mabanda ya Taasisi za Serikali kwenye uwanjwa wa maonyesho nanenane NGONGO na huduma kutolewa kuanzia saa 02:00 asubuhi – 11: 00 jioni.

Ewe, Mwananchi – Mkulima, Mvuvi na Mfugaji jitokeze Kusajiliwa kwani, Vitambulisho vya Taifa ni Ufunguo muhimu kwa maendeleo yako na Taifa kwa ujumla.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Taarifa Kwa Umma

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu