NIDA Yatunukiwa Cheti cha Mshindi wa Kwanza e-Mrejesho

Na. Hadija Maloya-Moshi

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imetunukiwa cheti cha ushindi wa kwanza kati ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kushughulikia malalamiko ya wananchi kwenye Mfumo wa e-Mrejesho.

Cheti hicho kimetolewa na Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni (Mb), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, wakati wa kufunga Semina Elekezi ya Viongozi Waandamizi wa Wizara hiyo, iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Viwanja vya Weruweru River Lodge vilivyopo Mkoani Kilimanjaro.

Akitunuku cheti hicho, Waziri Masauni amewapongeza NIDA kwa kushika nafasi ya kwanza kwa kazi kubwa ya kutoa mrejesho na kuwahudumia wananchi ikiwemo kutatua kero na malalamiko yao, kupokea ushauni, maoni na hata pongezi kutoka kwao kwa nyakati tofauti. “Nawapongeza kwa kupata ushindi wa kwanza, endeleeni kuwahudumia wananchi na kuzidi kuimarisha utendaji, ushirikiano na kudhibiti changamoto zilizopo na zitakazojitokeza kwa kuwa NIDA na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ujumla imebeba taswira ya Serikali na Wananchi” Alisema.

Sambamba na hilo, NIDA imetunukiwa cheti cha ushiriki wa mafunzo ya utumiaji wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kilichotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kwa kushiriki mafunzo hayo yenye lengo la kuwezesha Taasisi mbalimbali kutumia takwimu hizo ili kurahisisha utendaji na ushirikiano baina ya Taasisi.

Aidha, Mhe. Waziri amesisitizia Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano ndani ya Wizara pamoja na Sekta nyingine zilizopo nje ya Wizara. Vile vile amesisitizia suala la kutekeleza agizo la Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuwakutanisha viongozi waandamizi angalau mara moja kwa mwaka ili kufahamiana, kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu katika utendaji wa kazi zao.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ndugu Ally Gugu amemshukuru Waziri Masauni kwa kuridhia na kukubali kuja kufunga Semina hiyo, pamoja na kuzingatia agizo la Waziri Mkuu la kuwakutanisha Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwa niaba ya Viongozi Waandamizi hao, ametoa ahadi kwa Mhe. Waziri Masauni kuwa, baada ya semina hiyo watabadilika vya kutosha katika utendaji na kusimamia watumishi waliopo chini yao kutekeleza wajukumu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo ili kuendana na falsafa ya 4R iliyotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Semina Elekezi kwa Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imefanyika kwa muda wa siku mbili katika Viwanja vya Weruweru River Lodge huko Mkoani Kilimanjaro, ikiwa na kauli mbiu isemayo “Falsafa ya 4R ni Msingi wa Kujenga Usalama wa Raia na Mali Zao” Semina hiyo ilifunguliwa Septemba 06, 2024 na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo alisisitiza utendaji wa kazi kwa kutumia Falsafa ya Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga Upya Taifa, utekelezaji wa maelekezo ya Tume ya Haki Jinai na utumiaji wa nishati safi za kupikia ikiwemo umeme, gesi na makaa ya mawe. Aidha ilifungwa Septemba 07, 2024 na Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni (Mb), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kutoa vyeti vya Ushindi katika suala la kutatua kero na malalamiko pamoja na kutoa mrejesho kwa wananchi kwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, pamoja na Wizara yenyewe.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Ndugu Deusdedit Buberwa (kushoto) akipokea cheti cha ushindi wa kwanza ushughulikiaji malalamiko ya wananchi kwenye Mfumo wa e-Mrejesho kwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Ndugu Dorothy Mbenna (wa pili kushoto) akipokea cheti cha ushiriki wa mafunzo ya utumiaji wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ili kurahisisha utendaji na ushirikiano baina ya Taasisi.
Baadhi ya Wajumbe Menejimenti ya NIDA wakifuatilia utoaji wa vyeti kwa washindi wa e-Mrejesho kwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu