Mmuya Ahimiza Uwajibikaji Kazini

Na: Hadija Maloya – Dodoma

Watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wamehizwa kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii ili kuepuka uzembe, uvivu na migogoro katika utendaji kazi.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya alipokuwa anafungua kikao cha 25 cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika Januari 22, 2024 katika ukumbi wa Magereza Makao Makuu, Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu huyo amewasisitizia wajumbe wa Baraza kusimamia uwajibikaji na upatikanaji wa haki baina ya wafanyakazii na mwajiri kwa kuwa upatikanaji wa haki unaendana na utekelezaji wa wajibu wa kila mmoja “Baraza liwe chachu ya kuhimiza uwajibikaji na kusimamia upatikanaji wa haki kwa pande zote mbili, kwa kuwa hakuna haki inayopatikana bila ya kutimiza wajibu” alisema.

Alisema Baraza ni daraja la kuwaunganisha wafanyakazi na mwajiri. Aliwaelekeza kutumia nafasi hiyo kuunganisha pande hizo mbili ili kudumisha mahusiano bora kazini na kuboresha utendaji wa kazi.

Aliwaasa viongozi na wajumbe wote kwa ujumla kutotumia vyama vya wafanyakazi kuwa chanzo cha migogoro, wala kuchochea na kutetea uzembe na uvivu kazini.

Akizungumzia kuhusu zoezi la ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi, alielekeza watumishi wa NIDA kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapatiwa vitambulisho vyao kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na kusimamia ugawaji huo kwa weledi, uadilifu na uaminifu mkubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Eng. Ismail Rumatila alimshukuru Katibu Mkuu kwa nasaha alizotoa kwa watumishi. Aliahidi kuzifanyia kazi kwa vitendo ili NIDA na Serikali kwa ujumla iweze kutoa huduma za Usajili na Utambuzi wa Watu kikamilifu na  kukidhi haja za wananchi.

Akielezea utaratibu wa kuzalisha, kusambaza na kugawa Vitambulisho vya Taifa, Eng. Rumatila amesema takribani mikoa 21 imeshapelekewa na ugawaji unafanyika katika Ofisi za Serikali za Mitaa na Vijiji kwa muda unaoanishwa katika eneo husika ili kuwarahisishia wananchi kupata vitambulisho vyao karibu na maeneo wanayoishi, baada ya muda ulioanishwa kwisha, vitambulisho vitarejeshwa kwenye Ofisi za NIDA za wilaya na ugawaji utaendelea katika ofisi hizo.

 “Hivi sasa ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa unaendelea katika mikoa takribani 12 ya Tanzania Bara. Aidha, Mikoa mingine ipatayo tisa (9) inatarajiwa kufikishiwa vitambulisho hivi karibuni ili zoezi la ugawaji liendelee katika mikoa hiyo. Matarajio ni kuwa hadi kufikia Machi, 2024 watu wote wenye Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) wawe wamepata vitambulisho vyao nchi nzima” alisema.

Sambasamba na hilo, Eng. Rumatila ameainisha vipaumbele vilivyopitishwa na Baraza la Wafanyakazi katika kutekeleza Mpango wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kuwa ni pamoja na kuimarisha Usajili na Utambuzi wa Watoto, Raia, Wageni Wakaazi, Wakimbizi, Walowezi na Raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora); kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa watu waliokidhi vigezo.

Vipaumbele vingine ni kuongeza, kuimarisha na kuboresha miundombinu na usalama wa mifumo ya TEHAMA; kuboresha maslahi na mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Mamlaka; kujenga na kukarabati majengo ya ofisi, mitambo na kuimarisha upatikanaji wa hatimiliki za viwanja vya Mamlaka na kuimarisha na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa maduhuli na vyanzo vya mapato.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu