Na: Agnes Gerald – NIDA
Watumishi wapya wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) walioajiriwa hivi karibuni wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma ili kuleta tija na mafanikio kazini.
Akiwasilisha mada kwa watumishi wapya wa NIDA kuhusu Mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma Sura Na. 298, Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Mariam Kuhenga, Mhadhiri na Mwezeshaji toka Chuo cha Utumishi wa Umma amewahimiza kutii maelekezo wanayopewa na viongozi wao ikiwa ni pamoja na kuripoti katika vituo watakavyopangiwa haraka na bila kusita. “Ninawasihi mnapopewa maelekezo sahihi ni vyema mkatii na kutekeleza na siyo kukaidi kwani huo utakuwa ni utovu wa nidhamu”alisema Mariam.
Kwa upande wake Edson Guyai, Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Vitambulisho vya Taifa (NIDA) amewaasa Waajiriwa hao wapya 39 kutoa huduma kwa kuzingatia maslahi mapana ya umma na kuwahudumia vema wananchi wnaapofika katika vituo na ofisi za NIDA kwa lengo la kupata huduma za usajili na utambuzi wa watu.
Ameeleza kuwa Idara ya Uzalishaji Vitambulisho ni Idara Mama ambayo imebeba jukumu kuu ambalo NIDA tunapaswa kulitekeleza la Usajili, Utambuzi wa Watu, Utoaji wa Vitambulisho vya Taifa na Ushirikishanaji Taarifa za Utambuzi wa Watu kwa wadau wetu.
Amefafanua zaidi kwa kusema kuwa, Idara ya Uzalishaji Vitambulisho vya Taifa ina sehemu (sections) tatu: sehemu ya masuala ya Usajili na Utambuzi wa Watu, Uzalishaji Vitambulisho na ya Uhakiki na Usambazaji wa Vitambulisho vya Taifa ambapo matarajio ya Idara ni nguvu kazi iliyoongezwa na Serikali kuungana na iliyopo ili kuleta matokeo bora zaidi ya wananchi kuweza kuhudumiwa wengi kwa mara moja kama inavyotarajiwa na kwa ubora zaidi.
“Ninawasihi mjitoe kikamilifu katika kutekeleza majukumu yenu na kuwa tayari kujifunza mambo mapya kila siku ili kutofanya mambo kwa mazoea na kuwa wabunifu zaidi ili kuleta tija kwa Mamlaka” amesema Guyai.
Rainfrida Chinguille, Meneja Data amewataka watumishi hao kuzingatia matumizi sahihi ya huduma za TEHAMA huku Afisa Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Emmanuel Lugomoja, amewaeleza watumishi juu ya umuhimu wa kutambua stahiki zao kama watumishi wa umma tangu wanapoajiriwa, ikiwemo stahiki za likizo, uzazi, safari, kustaafu na nyinginezo nyingi.
Akizungumzia masuala ya Sheria, Osric Luoga, Afisa Sheria wa NIDA ameeleza juu ya Sheria za Utumishi wa Umma kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Usajili na Utambuzi wa Watu, inavyopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 39 walioajiriwa yameanza Juni 12 na yanafanyika katika ukumbi wa Mikutano wa NIDA Makao Makuu kwa siku nane na yatahitimishwa 21 Juni, 2023.