Usajili NIDA Kata kwa Kata Moro

Kuelekea Maadhimisho ya Mei Mosi 2023

Na: Agnes Gerald – NIDA

Ofisi ya Usajili ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wilaya ya Morogoro imeanzisha utaratibu wa kusajili Kata kwa Kata badala ya kwenda Tungi zilipo ofisi za NIDA ili kuwapunguzia umbali wananchi na kuhakikisha hakuna mwenye sifa ya kusajiliwa anayeachwa.

Ameyasema hayo Ndg. James Malimo, Afisa Usajili Mkoa wa Morogoro, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii ofisini kwake Tungi hivi karibuni kuelekea maadhimisho ya Mei Mosi, 2023.

Amesema ofisi za Usajili zilizoko mkoani Morogoro zimesogeza huduma za Usajili Kata kwa Kata ili kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi kuliko ilivyokuwa awali na kuongeza kwamba wameanza na Kata za Mafiga, Mkuyuni, Mtombozi, Kisemu, Mindu na Chamwino.

Katika jitihada za kusogeza huduma kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya mafanikio katika kuelekea katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, NIDA katika mkoa wa Morogoro inatoa huduma ya usajili kwenye Kituo cha Huduma Pamoja kilichopo Mafiga ambapo ni katikati ya mji, hivyo ni rahisi kufikiwa na wananchi kutoka pande zote za Morogoro. Taasisi nyingine zinazotoa huduma katika kituo hicho ni Uhamiaji, Ardhi, Benki na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Wenye mahitaji maalumu ni kundi muhimu katika jamii yetu ambapo ofisi ya Mkoa wa Morogoro haijawaacha nyuma bali imeweka utaratibu mzuri wa kuhudumia kundi hilo. Pindi wanaporipoti kwenye ofisi ya Usajili hupewa kipaumbele pasipo kulazimika kupanga foleni kutokana na hali yao kwani wengine ni wagonjwa wasioweza kusimama ama kuketi kwa muda mrefu” alisema.

Akiangazia upande wa changamoto wanazokabiliana nazo kiutendaji ameeleza kuwa ni pamoja na wananchi wengi kutokuwa na viambatisho vya kutosha na kutokuwa tayari kutoa ushirikiano pindi wanapopewa maelekezo. Aliwahimiza waombaji Utambulisho wa Taifa wa Morogoro kufuatilia vyeti vya kuzaliwa kwa rika zote.

Kuhusiana na uhakiki wa uraia, alieleza kwamba baadhi ya wananchi hawatoi ushirikiano wa kuanzia kwenye ofisi ya Uhamiaji iliyoko Msamvu badala yake wanawasilisha fomu za maombi kwenye ofisi ya NIDA, moja kwa moja hivyo kulazimika kurudishwa ili wakahakikiwe uraia kwanza.

Changamoto nyingine ni wananchi kutochukua vitambulisho vyao, akitolea mfano kwa walihitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mwaka 2018 ambao takribani 1800 hawajachukua vitambulisho vyao na kusema kuwa wanafunzi hao wanaweza kufika kwenye ofisi ya Usajili Morogoro mjini kuchukua vitambulisho vyao.

Aliongeza kwamba kama wahitimu wamehama makazi, wanaweza kuchukuliwa Kitambulisho na mtu mwingine kwa kumtambulisha kwa barua yenye majina matatu ya mmiliki wa Kitambulisho na ya anayetumwa, NIN na kusaini barua. Anayetumwa atatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa.

Amehitimisha kwa kuushukuru uongozi wa NIDA na Serikali kwa ujumla kwa kuwawezesha wananchi wa Mkoa wa Morogoro Kusajiliwa kwa zaidi ya asilimia 98% na amewahimiza wananchi katika mkoa huo kuendelea kujitokeza kwa wingi hususan katika maeneo ambayo huduma imesogezwa karibu.




A

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu