NIDA Yaadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani kwa Kusajili

  • Yajivunia kuwa Chachu ya Mageuzi Makubwa Nchini

Na: Agnes Gerald – NIDA

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeadhimisha Siku ya Utambulisho wa Taifa Duniani kwa Kusajili, Kutambua na Kugawa Vitambulisho vya Taifa.

 Hayo yamesemwa na Msemaji wa NIDA, Geofrey Tengeneza katika kilele cha kuadhimisha Siku ya Utambulisho wa Taifa Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Septemba 16.  

Alisema NIDA inatambua umuhimu mkubwa wa kuadhimisha siku hiyo kwani inatoa fursa kwa nchi zenye kutoa Utambulisho wa Taifa duniani, kutumia siku hiyo katika kuhamasisha na kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa raia na wageni wakaazi kujitokeza kusajiliwa na kutambuliwa ili wapatiwe Utambulisho wa Taifa unaowasaidia kutambulika kirahisi kitaifa na kimataifa.

Katika kuhakikisha kwamba huduma ya usajili na utambuzi inafanyika kwa urahisi, alisema hivi karibuni NIDA itatambulisha huduma ya Usajili wa Kielektroniki iliyokuwa ikisubiriwa kwa kipindi kirefu na wananchi ambapo sasa kiu yao imetimizwa kwani mwananchi ataweza kujaza fomu ya Utambulisho wa Taifa, kielektroniki.

“Mfumo huu wa usajili wa kielektroniki umetengenezwa na wataalamu wa ndani na umekamilika. Siku si nyingi utazinduliwa rasmi. “alisema. 

Akigusia historia ya kuanzishwa kwa suala la Utambulisho wa Taifa nchini, amesema, wazo la kuanzisha Vitambulisho vya Taifa kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoishi nchini Tanzania lilizaliwa mwaka 1968 katika kikao cha “Interstate Intelligence Gathering” kilichojumuisha wajumbe kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia. Kwa wakati huo nchi za Kenya na Zambia tayari zilikuwa na Vitambulisho vyao vya Taifa.

Iliazimiwa kwamba ili kuimarisha mahusiano ya kiusalama yanayozingatia   Utawala wa Sheria katika nchi hizo nne ni lazima nchi za Uganda na Tanzania nazo zikatoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia wao.

Baada ya azimio la kikao hicho, mwaka 1986 Serikali ilitunga Sheria ya Vitambulisho vya Taifa Na. 11 ambayo haikutumika wala kutungiwa kanuni zake hadi mwaka 2012 ndipo kanuni zilitungwa na kufanyiwa mapitio 2014 baada ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) mwaka 2008.

Shughuli ya Usajili na Utambuzi wa Watu ilianza mwaka 2011 kwa watumishi wa umma na baadaye ilipelekewa katika wilaya zote nchini.

Alisema hadi kufikia sasa NIDA imesajili wananchi zaidi ya milioni 24 (94 %,) imetoa Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) zaidi ya milioni 20 (85%) na Vitambulisho vya Taifa milioni 11 (51%) na zaidi.

Aliyataja baadhi ya manufaa ambayo yameletwa nchini na matumizi ya mfumo huo kuwa ni pamoja na kumwezesha mwananchi kusajili laini ya simu, kupata Namba ya Mlipa Kodi (TIN), kusajili biashara/kampuni – BRELA, kuomba hati ya kusafiria ya kielektroniki (e-Passport), kukata leseni ya udereva, kufungua akaunti ya benki, kukopesheka kirahisi kwenye taasisi za fedha, kuomba mkopo wa elimu ya juu, kujiunga na elimu ngazi mbalimbali, kuomba hati miliki ya kiwanja na nyumba. kujidhamini na kudhamini wengine na kupata huduma ya afya.

Aliyataja matumizi ya Kitambulisho cha Taifa kutokana na kuwa na kisilikoni (Cheap) kinaweza kutumika kama pochi ya kielektroniki (e-Wallet) ambako unahifadhi fedha na kufanya malipo kwa kutumia kitambulisho, kitambulisho kinaweza kutumika kama ATM CARD, kwenye maingio ya milango kielektroniki (e-Entrace), daftari la mahudhurio la kielektroniki (Electronic Attendance).

Uwepo wa kitambulisho cha kielektroniki kutasaidia wananchi kuondokana na adha ya kubeba utitiri wa vitambulisho kwani sasa taarifa zote muhimu zitapatikana katika Mfumo Mkuu wa Taifa wa Utambuzi wa Watu na  kinaweza kutumika kama hati ya utambuzi wa utaifa wa wananchi wanaovuka mipaka ndani ya nchi zilizoko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwingineko.

Kitambulisho cha Taifa vilevile kimechochea katika kuimarisha Utendaji Kazi Serikalini wenye matokeo chanya kwa kuwa na kumbukumbu sahihi za watumishi na malipo ya stahili zao, hasa wanapostahafu.

Habari picha: Wananchi na Watumishi wa umma wakisajiliwa, kutambuliwa na kupatiwa Vitambulisho vya Taifa, Dar Es Salaam, Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu