Marekebisho ya Tarehe au Mwezi au Mwaka wa kuzaliwa
Mwombaji yoyote anayehitaji kufanya mabadiliko ya tarehe au mwezi au mwaka wa kuzaliwa anahitajika kuwasilisha nyaraka zifuatazo:
Mabadiliko ya Taarifa ya Tarehe na Mwezi wa Kuzaliwa
a) Cheti cha kuzaliwa,
b) Ikiwa Mwombaji tayari alishawasilisha cheti chake cha kuzaliwa hapo awali wakati anasajiliwa na kuja kuwawasilisha cheti kingine kipya cha kuzaliwa chenye utofauti wa taarifa; Afisa Usajili husika anaweza kuomba uthibitisho wa nyaraka hiyo toka kwa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) na Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (The Zanzibar Civil Status Registration Agency-ZCSRA),
c) Mwombaji aambatanishe na nakala ya Tangazo kutoka katika Gazeti la Serikali lenye taarifa za mabadiliko husika,
d) Afisa Usajili Wilaya ili kutekeleza majukumu yake kwa usahihi anaweza akaomba nyaraka nyinginezo zozote zenye kuthibitisha taarifa/majina ya Mwombaji husika,
e) Mwombaji anapaswa kuchangia gharama ya kubadili taarifa husika shilingi 20,000/=, na iwapo makosa yamefanyika upande wetu, Afisa Usajili atajiridhisha na kuendelea na maboresho pasipo kulazimika kulipia gharama yoyote,
f) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kufanyiwa kazi na Maafisa Usajili wilaya.
Mabadiliko ya Mwaka wa Kuzaliwa
Maombi ya mabadiliko ya Mwaka wa Kuzaliwa hayatoruhusiwa isipokuwa yamepata kibali maalum kutoka kwenye Kamati ya Usajili na Utambuzi. Aidha, Mwombaji atatakiwa kuonyesha nyaraka zifuatazo; -
a) Cheti cha kuzaliwa kilichopatikana kipindi cha awali kilichotafutwa na Wazazi/Walezi,
b) Cheti cha kumaliza Shule ya Msingi,
c) Kadi ya Kliniki (CLINIC),
d) Cheti cha kumaliza shule za sekondari (Leaving Certificate),
e) Nyaraka yoyote ya awali yenye uthibitisho wa miaka ya mwombaji iliyopatikana kabla ya Kusajiliwa na Kutambuliwa na kupata Kitambulisho cha Taifa,
f) Mwombaji aambatanishe nakala ya Tangazo kutoka katika Gazeti la Serikali lenye taarifa za mabadiliko husika,
g) Afisa Usajili Wilaya ili kutekeleza majukumu yake kwa usahihi anaweza akaomba nyaraka nyinginezo zozote zenye kuthibitisha taarifa/tarehe ya Mwombaji husika,
h) Mwombaji anapaswa kuchangia gharama ya kubadili taarifa husika shilingi 20,000/= na iwapo makosa yamefanyika upande wetu, Afisa Usajili atajiridhisha na kuendelea na maboresho pasipo kulazimika kulipia gharama yoyote,
i) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kufanyiwa kazi ngazi ya awali na Maafisa Usajili wilaya kabla ya kuwasilishwa kwenye Kamati husika kwa Maamuzi.
Muhimu: - ombi la mteja linaweza kuafikiwa ama lah kutegemea na sababu na nia ya mteja kutaka kufanya maboresho ya taarifa zake