Na. Mwandishi wetu
Idadi kubwa ya Vitambulisho vya Taifa vilivyopokelewa katika ofisi ya Usajili ya Wilaya ya Ilala kutoka katika kituo cha Uzalishaji Vitambulisho cha NIDA kilichoko Kibaha Mkoani Pwani katika kipindi cha kuanzia mwaka 2012 hadi 2019, vimeshapelekwa katika ofisi mbalimbali za Serikali za Mitaa za Wilaya ya Ilala ili kuwapatia wahusika ambapo wananchi wengi wameshafika kwenye ofisi hizo kuchukua Vitambulisho vyao.
Kwa mujibu wa Kaimu Msajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Wilaya ya Ilala Bi. Zulfa Ally Mnyika amesema, vitambulisho ambavyo bado havijachukuliwa na wenyewe ni vichache na wanaendelea kuja kuvichukua japokuwa kasi ya kuvichukua si kubwa sana.
Bi. Zulfa aliyasema hayo wakati akielezea namna ofisi ya Usajili ya NIDA Wilaya ya Ilala inavyotekeleza majukumu yake kwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati Bw. Geofrey Tengeneza na Afisa Habari Bi. Hadija Maloya walipotembelea Ofisi hizo hivi karibuni ikiwa ni mwendelezo wa ziara yao ya kutembelea Ofisi za NIDA zilizopo Mkoani Dar es salaam.
Alisema awali wananchi walikuwa wakifika kwenye Ofisi za NIDA za Usajili Wilayani kuchukua vitambulisho vyao. Kwa hivi sasa huduma hiyo imesogezwa karibu na makazi ya wananchi ambapo Vitambulisho vya waombaji vikishazalishwa husambazwa kwenye ofisi za Serikali za Mitaa sambamba na kuwatumia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kwa njia ya simu ili wafike kuvichukua.
“Vitambulisho vichache vilivyosalia ofisini ni vile vya wananchi waliojisajili hivi karibuni kupitia BRELA, kundi la Watunishi wa Umma na Wanachuo. Niwaombe wahusika ambao bado hawajafika kuvichukua waje kuvichua hapa Ofisi ya NIDA iliyopo Mombasa Ilala” Alisema.
Akizungumzia zoezi la usajili Kaimu Msajili huyo wa NIDA Wilaya ya Ilala amesema zoezi hilo linaendelea vizuri na kwamba Kasi ya watu kuja ofisini kwa ajili ya zoezi la Usajili kwa sasa imepungua kwa kiasi kikubwa, kwani wanapokea kuanzia watu Sabini hadi themanini tu kwa siku ikilinganishwa na hapo awali ambapo kwa siku walikuwa wanapokea kuanzia watu 500 hadi 800. Amesema moja ya sababu ya kasi kupungua ni changamoto ya mlipuko wa virusi vya corona ambavyo vimeripotiwa kuathiri nchi mbalimbali duniani.
Katika ziara hiyo Maafisa hao walijionea shughuli mbalimbali zinavyofanyika, kuanzia wananchi wanavyopokelewa, wanavyopatiwa Fomu za Maombi ya Utambulisho wa Taifa, uhakiki wa Uraia unavyofanywa na Maafisa wa Uhamiaji, pamoja na taarifa zinavyoingizwa kwenye mfumo zikiwemo na za kibaiolojia (Biometric) kama vile uchukuaji alama za vidole, upigwaji picha na uwekaji wa saini ya kielektroniki. Aidha baada ya mwombaji kukamilisha Usajili, taarifa zake huchaakatwa na kuhakikiwa kwa mara ya mwisho ndipo Namba ya Utambulisho wa Taifa huzalishwa na hatimae Kitambulisho cha Taifa.
Wilaya ya Ilala ina ofisi mbili, moja iko Mombasa-Ukonga (Ofisi kuu ya Wilaya) na Ofisi ndogo iliyopo barabara ya Kivukoni kwenye Jengo la Magereza la zamani.
Tafadhali nilikua naomba kama kuna uwezekano wa kupata namba zangu za nida
Mwombaji wa Utambulisho wa Taifa baada ya kukamilisha Usajili, anaweza kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Taifa walau ndani ya muda wa kuanzia wiki na muda usiozidi mwezi iwapo ombi lake limeonekana kukidhi vigezo baada ya uhakiki kukamilika. Iwapo muda umezidi hapo uliza kwa Afisa Usajili katika ofisi ya NIDA, wilayani ili ujulishwe cha kufanya kwani yawezekana maombi yako yakawa na mapungufu kama vile kutokamilika kwa viambatisho n.k. Shukrani.