TANZANIA KUINGIA KWENYE UCHUMI WA KATI NI MATOKEO YA USIMAMIZI MZURI WA SERA ZA UCHUMI-KASSIM MAJALIWA

Na. Hadija Maloya

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa (MB), amesema kuwa mafanikio ambayo Tanzania imeyapata hivi karibuni ya kuingia katika kundi la nchi zenye uchumi wa kati duniani yametokana na usimamizi mzuri wa sera za uchumi nchini na hivyo kuifanya kuwa na uchumi imara.

Amewapongeza watanzania wote kwa juhudi na uchapakazi wao chini ya uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli ambao umeiwezesha nchi kupata mafanikio hayo ikiwa ni miaka mitano (5) kabla ya lengo lililowekwa la kufikia hatua hiyo mwaka 2025. Jumatano tarehe I Julai, 2020 Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilitangaza Tanzania kuingia kwenye uchumi wa kipato cha kati.

Mhe.Kassim Majaliwa ameyasema hayo wakati wa sherehe za ufunguzi rasmi wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba zilizofanyika leo tarehe 3 Julai, 2020 kwenye ukumbi wa Kobe uliopo ndani ya Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es salaam.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho hayo mwaka huu amewashukuru wafanyakazi, wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wajasiriamali na watanzania wote kwa ujumla wao kwa kuiunga mkono Serikali na kuiwezesha kuingia uchumi wa kipato cha kati. Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati ili kuongeza upatikanaji wa ajira na masoko, kukuza taasisi za Fedha ili ziendelee kutoa mikopo kwa masharti nafuu na rafiki katika kuendeleza na kukuza Viwanda hivi ili kuviwezesha kufanya kazi kwa tija zaidi.

Aidha, Mhe. Waziri Mkuu amesifu jitihada zilizofanyika kuwezesha Maonesho hayo kufanyika ndani ya muda mfupi baada ya kutangazwa kupungua kwa kiasi kikubwa maambukizi ya ugonjwa wa Corona.  Ameongeza kuwa kufanyika kwa maonesho haya ni ishara tosha kuwa Tanzania imefanikiwa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya COVID 19, na kwamba hilo limejidhihirisha katika maandalizi yaliyofanyika kwani yamezingatia kanuni za afya hasa katika kujikinga na maambukizi ya homa ya mapafu maarufu kama Corona inayoambukizwa na kirusi cha COVID 19.

“Janga hili la Corona limetoa funzo kwetu la kuimarisha sekta zetu mbalimbali hasa Kilimo, Biashara na Viwanda ili kuweza kujitosheleza na mahitaji ya chakula na ziada iweze kuuzwa nje ya nchi” alisema.  

Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (DITF) yenye kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” yanayofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 13 Julai, 2020 yamelenga kuboresha bidhaa kwa kutumia ubunifu na teknolojia za kisasa ili kuongeza thamani ya bidhaa, kutoa fursa kwa washiriki kutangaza na kutanua wigo wa masoko ya bidhaa zao, kutanua wigo wa ajira katika sekta mbalimbali hapa nchini ili kukuza Viwanda na kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akiwahutubia wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa sherehe za ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Dar es salaam (DITF) kwenye ukumbi wa Kobe uliopo ndani ya Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa Temeke, Jijini Dar es salaam.
Wageni waalikwa wakimsikiliza Mhe. Waziri Mkuu (hayupo pichani) wakati wa sherehe za ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Dar es salaam (DITF).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akikata utepe kwa ajili ya kuzindua kazi zilizobuniwa na taasisi za serikali wakati wa sherehe za ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya
Dar es salaam (DITF).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu