NIDA YAJIPANGA KUTOA HUDUMA WAKATI WA MAONESHO YA DITF

Na. Hadija Maloya

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Dar es Salaam International Trade Fair-DITF) maarufu kama Sabasaba yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai, 2020 katika uwanja waa Maonesho wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere uliopo barabara ya Kilwa, Manispaa ya Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati wa NIDA Bw. Geofrey Tengeneza amesema kuwa Mamlaka imeanza maandalizi ili kuiwezesha kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo na kwamba watayatumia pia maonesho hayo kutoa huduma ya Usajili na utambuzi wa watu hususan kwa wananchi wa mkoa wa Dar es salaam na vitongoji vyake.

Aliongeza kuwa Mamlaka ina nafasi na wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa wananchi wote wanaokidhi vigezo vya Usajili wanajisajili ili kuwawezesha kupata Namba za Utambulisho za Taifa ambazo watazitumia kwa matumizi mbalimbali.

“Tumejipanga kushiriki maonesho hayo ili kuwawezesha wananchi wote waliofikisha umri wa miaka 18 na zaidi na ambao hawajajisajili waweze kufanya hivyo kwa ajili ya kupata Namba za Utambulisho wa Taifa na hatimae Kitambulisho cha Taifa” alisema Bw. Tengeneza.

Ametoa rai kwa wananchi wote hususani ambao hawajajisajili na wale ambao hawajachukua namba za Utambulisho wa Taifa, kutembelea banda la NIDA wakati wa maonesho hayo ili wakamilishe Usajili wao na kujipatia Namba za Utambulisho wa Taifa.

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es salaam (DITF) hufanyika kila mwaka na kushirikisha mashirika, taasisi na makampuni mbalimbali ya serikali na binafsi ya hapa nchini na kutoka nje ya nchi. Maonesho hayo mwaka huu yamebeba ujumbe usemao “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu.”

Shughuli za usajili katika hatua mbalimbali zikiendelea kutolewa na NIDA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *