NIDA watakiwa kuwa waadilifu, wasiri

Na Agnes Gerald, NIDA

Watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na kutunza siri.

Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima alipofungua Baraza la Wafanyakazi Februari 24, 2020 katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Polisi, Dar es Salaam.

Amewataka watumishi wa NIDA kuzingatia maadili katika utekelezaji wa shughuli za Usajili za Mamlaka pindi wanapotoa huduma kwa wananchi. Amewataka Watumishi wa NIDA kufanya kazi kwa bidii ili wananchi wapatiwe huduma kwa wakati pamoja na kutunza siri za taasisi kwani kufanikiwa ama kutofanikiwa kwa NIDA kuko mkononi mwa kila mtumishi hivyo kila mtumishi asimame kwenye nafasi yake kwa kutimiza wajibu wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Dkt. Arnold Kihaule aliwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mamlaka hadi kufikia Desemba 2019 ambapo ameeleza idadi kubwa ya wananchi wameshasajiliwa na kupatiwa Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) ambazo zinatumika kusajili laini za simu, kufungua akaunti za benki, kukata leseni ya udereva, biashara, Kupata Namba ya Mlipa Kodi (TIN), kuomba ajira serikalini na huduma nyinginezo.

Aidha katika taarifa yake ameelezea baadhi ya changamoto zinazowakabili moja wapo ni kwa wananchi kutokuwa na viambata vya kutosha vya kuthibitisha uraia, umri na makazi na kueleza ambavyo NIDA imejitahidi kutoa elimu kwa umma katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Akizungumzia utaratibu wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Wafanyakazi Serikali Kuu na Afya (TUGHE), Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Tabu Mambo amewataka wajumbe kuhakikisha wanachagua Katibu wa Baraza kwa kufuata utaratibu, kumpima mgombea kama anatosha na kila mjumbe kuhakikisha anatumia haki yake ya msingi kupiga kura.

Vikao vya Baraza la Wafanyakazi serikalini vipo kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2002, Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma Na.19 ya mwaka 2003, pamoja na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004.

Watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakiimba wimbo wa Mshikamano Daima (Solidarity Forever) wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jeshi la Polisi Februari 24, 2020.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima akitoa maelekezo kwa Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakati akifungua kikao cha Baraza hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya  Jeshi la Polisi, Dar es Salaam Februari 24,2020.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Baraza hilo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dkt. Arnold Kihaule. Kailima alikuwa Mgeni Rasmi na alifungua kikao cha baraza hilo kilichofanyika  Februari 24, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam.

Comments on “NIDA watakiwa kuwa waadilifu, wasiri”

 1. TRYPHON JOSIAH says:

  Bukoba Manispa NIDA wapunguze matusi wakati wa kupokea watanzania, waelemishwe vizuri sio kutumia matusi katika maeneo ya ofisi. Kazi yao ni sawa na kazi zingine

  1. Nida says:

   Asante kwa taarifa itafanyiwa kazi

 2. SAID K. HAMAD says:

  Congratulation..

 3. MUSSA MGUZU says:

  hili suala la ukomo wa uraia tunaomba liangaliwe upya. tunatambua kuna watu kufa na kutoweka, kwa hili la kufa na kutoweka mamlaka za udhibiti wa taarifa kama hizi zihusike sana kwa mfano akifa mmoja kupitia majina yake taarifa za kifo zifike nida na nida wasitishe utambulisho wa marehemu, na kama mmoja atatoweka kupitia mipaka yetu mamlaka husika zifanye vivyo hivyo kwa kusitisha utambulisho, kwa dhana hii ya ukusanyaji wa taarifa za raia kuwa katika platform moja ni nzuri sana ila ukomo wa uraia uwe pale tu mtu anapofariki au kuhama nchi.

  1. Nida says:

   Ushauri umepokelewa

 4. victory godelo says:

  ujumbe umewaafikia kikubwa hapo waongeze bidi katika katika utendaji wao maana kumekua na tabia unamkuta mtumishi anachati na simu wakati wananchi wamekaa nje kwenye foleni yeye anachati na simu jamani yatupasa kujituma kadili ya uwezo wetu kuhudumia raia pale tunapokua maeneno ya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu